Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lamine aomba miaka 2 Yanga

LAMINE' Lamine aomba miaka 2 Yanga

Mon, 11 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ataka kujifunga hadi 2023, uongozi wampelekea Eymael, atoa neno...

HUKU Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, akisema kuwa klabu hiyo iko katika mkakati kabambe wa kuisuka timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao, beki wao kisiki, Mghana Lamine Moro amenogewa klabuni hapo na kuomba 'kufungwa' kwa miaka miwili zaidi.

Mwakalebela aliliambia Nipashe jana kuwa mkakati wao ni kuisuka klabu hiyo upya ili kujiuliza ni wapi walipojikwaa na kuukosa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa misimu mitatu mfululizo na wakati akiyasema hayo Lamine tayari ameomba kupewa mkataba wa miaka miwili zaidi ili kuwa sehemu ya mafanikio yajayo ya kikosi hicho.

Akithibitisha Lamine kuomba kuongezewa mkataba wa miaka miwili kutoka mmoja aliobakiza, Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli, alisema ni kweli beki huyo raia wa Ghana amewasilisha ombi hilo mezani kwao na kinachosubiriwa ni janga hili la corona kupita ili kukamilisha mchakato huo.

Bumbuli alisema, kimsingi Lamine amebakiza mkataba wa mwaka mmoja ambao unamalizika Julai 2021, lakini ameomba kuongezewa miaka miwili na tayari ombi hilo limefikishwa kwa uongozi na bila kuchelewa wakalifikisha kwa Kocha Mkuu, Mbelgiji Luc Eymael ambaye ameridhia beki huyo kuongezewa mkataba.

"Ni kweli kama mlivyoona kupitia akaunti yetu ya klabu kwamba Lamine Moro anatarajiwa kuongezwa mkataba wa kuitumikia Yanga hadi 2023, ameomba yeye mwenyewe na tumewasiliana na kocha amependekeza aongezwe.

"Kocha amesema Lamine bado ni mchezaji kijana na ana nguvu na uwezo wa kuendelea kuitumikia klabu kwa muda mrefu zaidi, hivyo amemkubali, kilichobaki ni uongozi kukaa baada ya janga hili la corona kupita na kumwongezea mkataba," alisema Bumbuli.

Lamine ambaye amezaliwa Februari 13, 1994 Accra nchini Ghana, amekuwa msaada mkubwa katika safu ya ulinzi ya Yanga ambapo kabla ya Eymael kutua, Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa alikuwa akimchezesha sambamba na Kelvin Yondani.

Hata hivyo, kutua kwa Eymael kulimfanya Yondani kupoteza namba kikosi cha kwanza na chaguo la Mbelgiji huyo likawa ni Juma Makapu na Lamine, ambao wamefanya kazi kubwa katika safu ya ulinzi ya timu hiyo ambayo imeruhusu mabao 20 tu kwenye mechi 27 ilizocheza wakati huu ikiwa na alama 51 katika nafasi ya tatu, ambazo ni pointi 20 nyuma ya vinara wa ligi hiyo, watani zao, Simba.

Tayari Yanga imemwongezea mkataba winga mshambuliaji wao, Mghana Bernard Morrison, huku ikielezwa wamefikia hatua nzuri na kiungo wao mkabaji Mkongomani Papy Tshishimbi anayemaliza mkataba msimu huu.

Lakini tangu kusimama kwa Ligi Kuu Machi 17, mwaka huu kutokana na janga la corona, Yanga imekuwa ikihusishwa na usajili wa nyota kibao kutoka nje na ndani ya nchi.

Baadhi ya wachezaji ambao Yanga imekuwa ikihusishwa na kuhitaji huduma zao ni pamoja na kiungo wa Timu ya Taifa ya Rwanda (Amavubi) na Rayon Sports, Ally Niyonzima, kiungo mkabaji wa FC Kariobangi Sharks, Mkenya Yidah Sven, mshambuliaji Reliants Lusajo wa Namungo FC na beki wa kati wa Coastal Union, Bakari Mwamnyeto.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live