NYOTA wa Simba Erasto Nyoni, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na Mzamiru Yassin kila mmoja amesisitiza kwamba moto ni ule ule.
Tshabalala nahodha msaidizi alisema, mbali na kutolewa kimataifa lakini wanamshukuru Mungu kwa hatua waliyofikia kwa kuwa ilikuwa ni lazima mmoja atoke ili mwingine aende.
“Sisi sasa hivi akili zetu ni mchezo na Dodoma Jiji halafu na mechi za Ligi Kuu zilizosalia maana huko Ligi ya Mabingwa kumepita,” alisema Tshabalala.
Huku Mzamiru akiwataka Wanasimba kuendelea kuwaunga mkono katika michezo ya nyumbani ili kupata matokeo mazuri ambayo yatawapa nafasi ya ushiriki wa michuano hiyo mwakani.
“Yaliyopita yamepita, tumeumia sana, ila ndio mpira, sasa tunageukia majukumu mengine kuhakikisha tunafanya vizuri zaidi,” alisema Mzamiru.
Upande wa Nyoni alisema, kwa sasa kila mchezaji anajua wanapambania nini baada ya kupoteza upande huo ambapo wanaanza na Dodoma Jiji.
“Tutapambana kuhakikisha tunafanya vizuri mechi zetu zote za Ligi na hata FA tutimize malengo yetu ya kuyatetea mataji yote mawili ambayo tumeyashikilia,” alisema Nyoni.
Nyota hao wa Simba jana walifanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wao wa Mo Simba Arena uliopo Bunju na miongoni mwa nyota waliokuwepo ni Perfect Chikwende ambaye anacheza mechi za Ligi Kuu na Shirikisho pekee.