Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwa Mzungu mnapigwa nyingi

90037 Mzungu+pic Kwa Mzungu mnapigwa nyingi

Sat, 28 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

MACHALIII wa AFC Arusha walipopigwa mabao 6-0 kwenye mechi ya Kombe la FA, kuna baadhi ya mashabiki waliponda wakiamini Simba ilibahatisha tu kwa vile mayanki wa Arachuga walikuja kichovu, lakini ukweli Simba hii ya Kocha Sven Vanderbroek ukiingia kichwa kichwa unaumbuka!

Inaonekana kocha huyo kutoka Ubelgiji amekuwa na falsafa yake ya kugawa dozi nene kwa kila timu pinzani anayokutana nayo baada ya jana Jumatano kuwanyoosha Lipuli FC kwa mabao 4-0 katika mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu Bara na kumfanya ndani ya dakika 180 tu Sven avune mabao 10.

Utamu zaidi ni kwamba dozi hizo anagawa wakati akisaliwa na mechi mbili tu kabla ya kuvaana na watani wao za jadi, Yanga mchezo utakaopigwa Uwanja wa Taifa, siku ya Januari 4.

Ikiwa nyumbani, Simba ilipata ushindi wa kwanza jijini Dar es Salaam na wa pili dhidi ya Lipuli tangu timu hiyo ya Iringa ilipopanda Ligi Kuu 2017, huku straika wake Meddie Kagere akiongeza idadi ya mabao yake baada ya kufunga moja na kufikisha tisa, ilhali Hassan Dilunga ‘HD’ akitakata uwanjani hapo.

Katika mchezo huo ambao kabla ulitarajiwa kuwa mgumu kwa Simba kutokana na rekodi za mechi zao nne zilizopita dhidi ya Lipuli, lakini kuonyesha mambo yamebadilika chini ya Sven na Seleman Matola aliyewahi kuinoa Wanapaluhengo walienda mapumziko wakiwa mbele kwa bao 1-0, huku ikitawala mchezo huo kwa soka safi.

Simba iliuanza mchezo huo kwa kasi na dakika ya 6 beki wake wa kushoto Gadiel Michael alitengeneza shambulizi zuri lakini krosi yake akimtafuta Kagere ilidhibitiwa vyema na kipa wa Lipuli, Agathony Anthony.

Wageni walijibu mashambulizi dakika ya 9 shuti kali la kiungo Kenneth Masumbuko akiwa nje ya eneo la hatari lilipanguliwa vyema na kipa Beno Kakolanya na kuwa kona iliyokosa madhara.

Sven alifanya mabadiliko ya wachezaji wanne katika kikosi kilichoisambaratisha AFC, akiwachomoa Haruna Shamte, Gerson Fraga, Deo Kanda na Ibrahim Ajibu na kuwaanzisha Gadiel, Jonas Mkude, Hassan Dilunga na Shiboub Sharrafeldin.

Vinara na watetezi hao wa Ligi Kuu walipata bao la kuongoza dakika ya 11 likifungwa kwa umakini kwa shuti safi akipokea krosi safi ya beki wa kulia Shomari Kapombe aliyepandisha mashambulizi.

Timu zote zilifanya mashambulizi ya kupokezana katika dakika zaidi ya 30 zilizosalia kabla ya kwenda mapumziko, huku Lipuli wakionekana kulisaka bao la kusawazisha bila mafanikio.

Kipindi cha pili Simba walirudi na nguvu na dakika ya 49 Kagere alifunga bao la pili akimfunga kirahisi Agathony aliyedhani mfungaji huyo ameotea akipokea pasi ya Chama.

Wakati Kagere akienda kufunga mabeki wa Lipuli walisimama wakimuangalia mwamuzi msaidizi Kassim Safisha kutoka Pwani kama atanyoosha kibendera lakini haikuwa hivyo.

Baada ya kukosa mabao mengi ya wazi, Dilunga alifunga bao kwa penalti dakika ya 57 baada ya mwamuzi Martin Saanya kuamuru kwa madai Lufunga aliunawa mpira wakati Chama akitaka kufunga mpira uliogonga mwamba. Penalti hiyo ililalamikiwa na wachezaji wa Lipuli.

Dakika ya 62 Simba ilifanya mabadiliko ya kuwatoa Jonas Mkude na Kahata na kuwaingiza Mzamiru Yassin na Deo Kanda.

Mabadiliko hayo yaliisaidia Simba kwani Dilunga kufunga bao lake la pili na la nne kwenye mchezo huo akipokea pasi safi ya Sharaf Shiboub.

Ushindi huo umeifanya Simba kuzidi kujikita kileleni ikifikisha alama 28 baada ya mechi 12 na mabao 23, huku Lipuli wakiporomoka kutoka nafasi ya nane hadi ya 10 wakisaliwa na alama zao 18 sawa na Yanga ila sasa wakiwa nyuma ya Vijana wa Jangwani kwa tofauti ya uwiano wa mabao tu.

SIMBA: Kakolanya, Kapombe, Gadiel, Tairone, Wawa, Mkude, Dilunga, Shiboub, Kagere, Chama, Kahata

LIPULI: Agathony, Kameta, Kichiba, Majige, Lufunga, Tangalo, Mwinyi, Mgayu, Nonga, Saliboko na Masumbuko.

Chanzo: mwananchi.co.tz