Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kumbe kuna Serengeti Boys nyingine ya ‘Ulaya’!

14108 Pic+serengeti TanzaniaWeb

Tue, 28 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Achana na matokeo ya kufungwa 3-1 na Uganda katika nusu fainali, kikosi cha Serengeti Boys, kimekuwa gumzo kutokana na kandanda safi wanalotandaza katika mashindano ya kuwania nafasi ya Afcon U17, yanayoendelea kutimua vumbi nchini kwa ukanda wa Afrika mashariki na kati.

Awamu ya kwanza kwa Serengeti Boys ambayo ipo chini ya kocha mkuu, Oscar Milambo kutandaza soka safi ilikuwa nchini Burundi katika mashindano ya Cecafa U-17 ambako walitwaa ubingwa baada ya kuwalaza Somalia mabao 2-0 katika fainali.

Vijana hao walianza kuonyesha kandanda la kuvutia kwenye mchezo wao wa kwanza katika mashindano hayo dhidi ya Uganda waliotoka nao sare ya bao 1-1, lakini mechi ya pili wakailaza Sudan mabao 6-0.

Katika hatua ya nusu nusu fainali, Serengeti Boys walipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Kenya katika mchezo uliopigwa katika uwanja wa Muyinga na baadaye kutwaa ubingwa.

Kabla ya kufungwa kwenye nusu fainali, ilizifuynga Burundi 2-1, Sudan 5-0 na Rwanda 4-0.

Asilimia kubwa ya kikosi cha Serengeti Boys iliundwa na wachezaji wa ndani lakini hapa, Jarida la Spoti Mikiki kama kawaida linakuletea nyota wa Kitanzania wenye umri chini ya miaka 17 ambao wapo kwenye akademi mbalimbali za soka kuanzia Afrika hadi Ulaya.

Nyota hao wanaweza kukiongezea nguvu kikosi cha Serengeti Boys katika Fainali za Afcon ambazo mwakani Tanzania inakuwa mwenyeji.

Samweli George/ Jomo Cosmos, Afrika Kusini

Anamudu kucheza nafasi ya kiungo mchezeshaji au winga wa kushoto na kulia atatimiza miaka 17 mwakani, kinda huyo yupo kwenye kikosi cha vijana cha Jomo Cosmos ya Daraja la Kwanza Afrika Kusini.

Suleyman Juma ‘Aguero’/Royal Lions, Afrika Kusini

Juma ni mshambuliaji mwenye umri chini ya miaka 17 ambaye yupo kwenye Kituo cha Royal Lions cha Afrika Kusini na ndoto yake ni siku moja kuwa mchezaji wa daraja la juu kama ilivyo kwa Mbwana Samatta.

“Afrika Kusini kuna mtandao mkubwa kwa wachezaji kupata nafasi ya kwenda Ulaya tofauti na nyumbani Tanzania naamini muda ukifika kila kitu kitakuwa sawa,” anasema Aguero.

Roberto Nditi/ Reading, England

Roberto (17) ambaye ni mdogo wa Adam Nditi anayekichezea kikosi cha vijana cha Reading chenye umri chini ya miaka 18 angeweza kuanza kutumika kwenye kikosi cha Serengeti Boys kutokana na kuzaliwa kwake Oktoba Mosi, 2000.

Kuanza kulitumikia Taifa tangu ngazi ya chini kungetengeneza mazingira ya kutompoteza mchezaji huyo ambaye amekuwa akifanya vizuri upande wa Ligi Kuu ya vijana nchini England.

Roberto ni beki wa kati mwenye matumizi mzuri ya nguvu na akili na ndiyo maana msimu uliopita licha ya umri wake mdogo aliombwa kuwaongezea nguvu kikosi cha Reading cha vijana wenye umri chini ya miaka 21.

Zion na Paolo Nditi/ Reading, England

Zion na Paolo ni watoto pacha wa Nditi ambao wanaumri wa miaka 13, wadogo hao wa Adam aliyewahi kuwa Chelsea kabla ya kupotea kwenye soka, wapo kwenye akademi ya Reading na kaka yao Roberto ambaye wanatofautiana naye daraja.

Adrian Kitare/ Barcelona, Hispania

Kitare anaweza kuiongezea nguvu Serengeti Boys ya mwakani kama ataaminiwa na kupewa nafasi hiyo, kinda huyo wiki chache zilizopita alitoka kufanya majaribio ya kujiunga na akademi ya FC Barcelona ‘La Masia’.

Kupata nafasi ya kufanya majaribio La Masia lazima mchezaji awe na ushawishi wa uwezo siyo kila mchezaji anaweza kupata nafasi ya kufanya majaribio kwa maana hivyo Kitare kwa umri wake anaweza kushirikiana vyema na Kelvin John anayefanya vizuri kwa sasa kwenye kikosi hicho.

Nasry Aziz/ Aspire, Senegal

Nasry (17) ambaye amewahi kuitwa kwenye kikosi cha Ngorongoro Heroes ana umri ambao utamfanya mwakani kucheza michuano ya mataifa ya Afrika.

Winga huyo wa kituo akademi ya Aspire Football Dream iliyopo katika mji wa Dakar nchini Senegal atatimiza miaka 18 baada ya kumalizika kwa michuano hiyo.

Malimi Majaliwa/ Man City Academy, England

Malimi mwenye umri chini ya miaka 15, aliitwa kwa mara nyingine na Manchester City baada ya kufanya majaribio ya wiki moja miezi kadhaa nyuma na kuambiwa asubiri majibu ya majaribio hayo.

“Kucheza Ulaya ni ndoto yangu na nashukuru sana wazazi wangu nyumbani na familia kwa ujumla kwa kunisapoti na nimetoa ahadi kwao kuwa sintowaangusha upande wa masomo, itakuwa ajabu kuwa mchezaji nisiye na elimu kichwani,” anasema kinda huyo.

Rashidi Udikaluka/ Spittal, Austria

Udikaluka ambaye ni kiungo wa Spittal ya Austria anaumri wa miaka 17, kinda huyo atatimiza miaka 18, Juni 13 kwa maana hiyo atakuwa na uwezo wa kukiongezea nguvu kikosi cha Serengeti Boys ambacho kitachuana kwenye Afcon, Mei 12 hadi 26 mwakani.

Chanzo: mwananchi.co.tz