Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kuiona Taifa Stars, Equatorial Guinea buku tatu tu

83194 Pic+stars Kuiona Taifa Stars, Equatorial Guinea buku tatu tu

Sat, 9 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetangaza kiingilio cha Sh 3,000 na Sh 5,000 kwa mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2021 kati ya Taifa Stars na Equatorial Guinea utakaochezwa Novemba 15, kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam kuanzia saa 1.00 usiku.

Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao alisema tiketi za Sh3,000 kwa mashabiki watakaokaa katika viti vya majukwaa ya kijani wakati viti vya rangi ya bluu na machungwa bei ya tiketi itakuwa ni Sh 5,000.

"Kuelekea mechi hiyo dhidi ya Equatorial Guinea, TFF imeweka viingilio vya chini ili kutoa nafasi kwa mashabiki wengi kujitokeza kushangilia.

“Masuala ya ufundi yanabakia kwa benchi la ufundi. Mchezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania anapokuwa amevaa jezi ya Taifa Stars ni wajibu wetu kumshangilia," alisema Kidao.

Mwenyekiti wa kamati ya hamasa ya Taifa Stars, Haji Manara aliwaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi katika mchezo huo ili kuutumia kama pongezi kwa nahodha Mbwana Samatta na kikosi kiujumla.

"Jana Samatta amefanya jambo kubwa na la kipekee kwa kufunga bao kwenye Uwanja wa Anfield dhidi ya Liverpool. Ni vyema tukajitokeza kwa wingi iwe ishara ya kumpongeza kwa kile alichokifanya. “Tangu timu yetu ya taifa ilipofuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (Chan) hatujapata nafasi ya kuwapongeza kama nchi hivyo tuutumie mchezo wetu dhidi ya Equatorial Guinea kutimiza hilo," alisema Manara.

Mwenyekiti wa chama cha mashabiki wa soka Tanzania, Karigo Godson alisema hamasa ya mashabiki ina nafasi kubwa ya kuipa matokeo chanya Stars.

"Mashabiki tunapojitokeza kwa wingi na kuwashangilia vijana wetu, wanapata hamasa na kujituma zaidi," alisema Karigo.

Chanzo: mwananchi.co.tz