Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kuelekea Afcon - U17 hii ndio goldern Eaglets ya Nigeria

43611 Pic+afcon Kuelekea Afcon - U17 hii ndio goldern Eaglets ya Nigeria

Mon, 25 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wakati maandalizi ya kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) kwa Vijana chini ya miaka 17 yakizidi kupamba moto kwa timu shiriki, leo tunaiangazia Nigeria.

Fainali hizo zitakazofanyika kuanzia Aprili 14-28 na washindi wawili wa kila kundi watafuzu nusu fainali lakini pia watakata tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia kwa vijana kutoka Afrika zitakazofanyika Oktoba nchini Peru.

Tanzania inayowakilishwa na Serengeti Boys, imepangwa Kundi A pamoja na Uganda, Angola na Nigeria wakati Kundi B lina timu za Cameroon, Senegal, Morocco na Guinea.

Timu ya vijana ya Nigeria inayojulikana pia ‘Golden Eaglets’ itafungua pazia la fainali hizo dhidi ya Serengeti Boys.

Nigeria ambayo inasifika kwa timu za vijana, pia ni moja ya timu alikwa katika mashindano maalumu ya vijana yatakayofanyika kuanzia Machi 1-10 nchini Uturuki.

Mashindano hayo maalumu ya Uturuki yanashirikisha timu zote nane zilizofuzu Afcon ya vijana na nne za Ulaya.

ILIVYOFUZU

Nigeria maarufu kama ‘Golden Eaglets’ imefuzu kucheza Fainali za Afcon baada ya kubeba ubingwa wa Kanda B wa mashindano ya kufuzu kwa nchi zinazounda Kanda ya Soka ya Afrika Magharibi.

Ilimaliza ikiwa nafasi ya kwanza kwenye Kundi B lililokuwa pia na timu za Burkina Faso,Ivory Coast,na Benin na ikaja kuichapa Niger kwenye nusu fainali kwa mabao 2-1 na mchezo wa fainali ikabuka na ushindi wa penalti 3-1 dhidi ya Ghana baada ya kutoka nayo sare ya bao 1-1 kwenye dakika 90.

MAFANIKIO

Timu ya vijana ya Nigeria imeshiriki fainali za Afrika za U-17 mara nane ambapo kati ya hizo, imetwaa ubingwa mara mbili mwaka 2001 na 2007 na kumaliza katika nafasi ya pili mara mbili.Pia imemaliza nafasi ya tatu mara moja na nafasi ya nne mara moja.

Pia timu hiyo imeonekana ni moja ya timu tishio kwani imewahi kutwaa ubingwa wa Dunia mara tano mwaka 1985, 1993, 2007, 2009, 2013 na 2015 na imemaliza kwenye nafasi ya pili mara tatu.

Timu hiyo pia ni chimbuko la mastaa wengi wa soka waliotamba Duniani kama Jay Jay Okocha, Celestine Babayaro, John Obi Mikel, Kelechi Iheanacho na wengineo wengi.

KIKOSI KILIVYO

Kikosi cha Nigeria kinaongozwa na kocha Manu Garba mwenye miaka 53 na amewahi kuipa ubingwa wa Dunia timu hiyo mwaka 2013 na mwkaa 2015 aliiwezesha timu ya vijana chini ya miaka 20 kutwaa ubingwa wa Afrika.

Kikosi cha timu hiyo kinaundwa na makipa Joseph Oyomide,John Amah na Joseph Essien wakati mabeki ni Muhammad Ibrahim,Samson Tijani,David Ishaya, Clement Ikenna, Adam Mustapha na Sunday Odey.

Viungo ni Ibraheem Jabaar,Olatomi Olaniyan,Babatunde Akinsola na Peter Agba wakati washambuliaji ni Oluwatimilehin Adeniyi, Olankule Olusegun na Favour Akem.

Kocha Garba anapambana kumjumuisha katika kikosi chake kipa Joseph Oluwabusola ambaye ana umri chini ya miaka 16 na aliyekuwa kipa namba moja wakati wa mashindano ya kufuzu Afcon yaliyofanyika nchini Niger.

Kipa huyo anaichezea timu ya vijana ya klabu ya Bournemouth side iliyopo nchini England lakini ratiba ngumu ya shule imemfanya kushindwa kujiunga na kambi ya timu yake ya Taifa.

WACHEZAJI HATARI

Mshambuliaji, Olankule Olusegun ndiye anayeonekana mchezaji tishio zaidi katika kikosi cha Nigeria kwani katika mashindano ya kufuzu aliifungia Nigeria mabao matatu.

Mashambuliaji huyo ana nguvu na kasi huku akiwa imara katika kupiga mashuti ya mbali na kutoa pasi za mabao kwa wenzake.

Wachezaji wengine hatari katika kikosi hicho ni viungo Peter Agba na Babatunde Akinsola.



Chanzo: mwananchi.co.tz