Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kombe la shirikisho afrika, Yanga chaguo moja tu basi

82741 Pic+yanga Kombe la shirikisho afrika, Yanga chaguo moja tu basi

Mon, 4 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mambo matatu yanaiweka Yanga kwenye wakati mgumu kuibuka na ushindi ugenini leo huko Misri, na pengine kuitupa nje ya mashindano Pyramids, ingawa kwenye soka lolote haliwezi kuwa jambo la ajabu kutokea.

Matokeo ya mchezo wa kwanza nyumbani wiki moja iliyopita, kiwango duni ambacho imekuwa ikionyesha katika mechi zake pamoja na unyonge ugenini dhidi ya timu za Misri kuelekea mechi hiyo itakayochezwa katika Uwanja wa Al Salam jijini Cairo leo kuanzia saa 3.00 (kwa muda wa Tanzania), vinaipa Yanga mlima mrefu wa kupanda mbele ya Pyramids.

Kipigo cha mabao 2-1 ambacho ilipata katika mchezo wa kwanza uliocheza nyumbani Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, yanailazimisha kusaka ushindi wa kuanzia mabao 2-0 ili iweze kutinga hatua ya makundi ya mashindano hayo.

Kwa maana hiyo wawakilishi hao wa Tanzania watalazimika kutumia nguvu na hesabu kubwa za kuhakikisha wanafunga mabao na kuwazuia wapinzani wao wasipate mabao.

Hata hivyo, Pyramids huenda wakacheza bila presha kubwa kwani wanahitaji matokeo ya sare au ushindi wa aina yoyote ili waweze kusonga mbele.

Lakini ukiondoa presha ya matokeo ya mechi ya kwanza, kiwango kisichoridhisha cha Yanga ambacho imekuwa ikionyesha kwenye mechi za msimu huu ni suala lingine ambalo linaleta hofu ya uwezekano wa kuibuka na ushindi katika mchezo huo. Udhaifu wa safu ya ushambuliaji ya timu hiyo katika kutumia nafasi ambazo imekuwa ikizipata kufunga mabao na vilevile makosa ya mara kwa mara ambayo imekuwa ikiyafanya kujilinda ni changamoto kubwa watakapokuwa wanaikabili Pyramids.

Timu hiyo ya Misri imeonekana kuwa bora kung’amua na kutumia udhaifu wa timu pinzani kufunga mabao ambayo yamekuwa chachu kwao kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali.

Pamoja na hayo, rekodi zisiyoridhisha za Yanga katika mashindano ya kimataifa pindi inapokuwa ugenini kukabiliana na timu za Misri huenda zikaweka wapinzani wao katika hali nzuri kisaikolojia tofauti na wao, kwani haijawahi kupata ushindi wala sare katika mechi zote ilizocheza huko.

Yanga imecheza mechi tisa dhidi ya klabu za Misri ugenini na kufungwa zote, huku ikifunga bao moja na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 26.

Lakini kiujumla imekuwa ikipata wakati mgumu pindi inapocheza na timu kutoka Kaskazini mwa Afrika kwenye mataifa yanayozungumza Kiarabu.

Yanga imecheza mechi 16 ugenini dhidi ya klabu za huko ambapo haijawahi kupata ushindi, imetoka sare moja na kupoteza michezo 15. Timu hiyo imefunga mabao mawili na imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara 45.

Hakuna mabadiliko makubwa ambayo benchi la ufundi la Yanga linaweza kuyafanya na ni sura chache ambazo zinaweza kuanzishwa katika kikosi cha kwanza, huku wengi ambao walianza katika mechi iliyopita wakitarajiwa kuwa kikosini.

Katika safu ya ulinzi, Lamine Moro ataingia kuchukua nafasi ya Kelvin Yondani ambaye anatumikia adhabu ya kadi na huenda mshambuliaji Juma Balinya akaanzishwa kuchukua nafasi ya Mrisho Ngassa.

Nidhamu katika kujilinda na kushambulia ni silaha kubwa inayoweza kuibeba Yanga vinginevyo inaweza kujikuta kwenye wakati mgumu mbele ya Pyramids.

Hata hivyo, kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera alisema kuwa timu yake inaamini kwamba ina nafasi ya kuishangaza Pyramids katika mchezo wa leo.

“Mpira ni mchezo wa kushangaza. Lolote linaweza kutokea na jambo la msingi ni wachezaji kuhakikisha wanacheza kwa umakini na utulivu wa hali ya juu katika dakika zote za mchezo. Kama wao waliweza kupata ushindi hapa hata sisi tunaweza kupata ushindi kule,” alisema Zahera.

Kwa Yanga, matokeo mazuri katika mchezo huo yanaweza kuwa chachu ya kupandisha ari kikosini kwa ajili ya michuano ya Ligi Kuu Bara ambapo iko nafasi ya 15.

Chanzo: mwananchi.co.tz