Kocha mkuu wa timu ya taifa ya riadha, Suleiman Nyambui kesho Jumatano atakuwa miongoni mwa wanariadha mashuhuri wadunia waliopewa heshima ya picha zao kuwekwa kwenye Hall of Fame wiki hii.
Nyambui yuko Marekani tangu wiki iliyopita kwa mualiko maalumu wa Chama cha Makocha wa riadha kwenye vyuo vikuu vya nchi hiyo akishiriki kwenye hafla ya kutambua mchango wa nyota wa zamani waliowahi kuvitumikia kwa mafanikio vyuo vikuu vya nchi hiyo kwenye michezo.
"Nilipata ofa ya masomo Marekani kutokana na riadha na kuitumiki nafasi hiyo kwa mafanikio makubwa hadi sasa kuwa miongoni mwa nyota ambao tumealikwa kwenye hafla ya tuzo itakayokwenda sanjari na kushuhudia mashindano makubwa ya vyuo vikuu vya hapa yatakayofanyika Jumatano," amesema Nyambui.
Amesema moja ya heshima ambayo amepewa i picha yake kuwekwa kwenye Hall of Fame na rekodi zake, wametembelea pia uwanja wa kimataifa ambako mashindano ya dunia ya mwaka huu yatafanyika kwenye jimbo la Oregon mji wa Eugene.
"Jumatano nimealikwa pia kushuhudia mashindano ya vyuo vikuu na kupewa nafasi ya kuutubia katika mashindano hayo makubwa ya vyuo vikuu," amesema.