Kigali. Kocha Mwinyi Zahera ameanza kazi rasmi Yanga baada ya kukaa kwenye benchi la timu hiyo kwa mara ya kwanza tangu alipojiunga na klabu hiyo kongwe nchini.
Zahera licha ya kuanza kuifundisha Yanga hakuwa akikaa kwenye benchi baada ya kukosa kibali cha kufanya kazi ambacho alikabidhiwa juzi.
Kwa mara ya kwanza Zahera alianza kuzungumza na waandishi wa habari juzi katika mkutano wa kujiandaa na mechi dhidi ya Rayon Sports iliyochezwa jana.
Noel Mwandila alikuwa akiongoza benchi la timu hiyo katika mechi mbalimbali ikiwemo ya Ligi Kuu Tanzania Bara walioshinda mabao 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar.
Mratibu wa Yanga Hafidh Saleh alisema mchezo dhidi ya Rayon Sports ulikuwa wa kwanza kwa Zahera kukaa kwenye benchi.
Hafidh alisema Zahera ataendelea kukaa kwenye benchi katika mechi za Ligi Kuu baada ya kupata vibali vya kufanya kazi nchini.
“Kocha ataanza leo (jana) kukaa kwenye benchi kila kitu kimekamilika na Rayon ilikuwa mechi ya kwanza na ataendelea na kazi ya kuongoza benchi la ufundi,”alisema Hafidh.