Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kocha Simba SC ageukia Waarabu

44925 Pic+simba Kocha Simba SC ageukia Waarabu

Tue, 5 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati kikosi cha Simba kikiondoka leo jioni kwenda Algeria, Kocha Patrick Aussems, ametaja mambo matatu ya kuiua JS Saoura katika mchezo wao wa Jumamosi wiki hii.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Aussems alisema jambo la kwanza amekiandaa kikosi chake kucheza mchezo wa kufunguka licha ya kucheza ugenini kwa kuwa anahitaji pointi tatu muhimu.

Alisema atawatumia washambuliaji ‘pacha’ John Bocco na Meddie Kagere kufunga mabao kwa kutumia mfumo huo ambao ameuandaa. Aussems anatumia zaidi mfumo wa 4-4-2.

Pia alisema ametoa maelekezo kwa mabeki wake namna ya kupambana na wapinzani wao kuhakikisha hakuna mabao yanayofungwa katika mchezo huo.

Simba inatarajiwa kucheza mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na JS Saoura ya Algeria Jumamosi wiki hii ikiwa na mtaji wa mabao 3-0 iliyopata katika mchezo wa kwanza Dar es Salaam.

Simba ilifungwa mabao 5-0 na AS Vita ya DR Congo na baadaye ilinyukwa idadi kama hiyo na Al Ahly ya Misri. Mechi zote mbili ilicheza ugenini.

Alisema pamoja na kufungwa idadi kubwa ya mabao, jicho lake lipo kwa Bocco na Kagere aliodai wamekuwa na maelewano mazuri katika safu ya ushambuliaji.

Wakati Bocco ambaye ni nahodha amefunga mabao tisa, Kagere raia wa Rwanda amepachika 12 katika mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kocha huyo raia wa Ubelgiji, alisema atawatumia nyota hao na wengine aliowaandaa kupata matokeo mazuri ingawa anatarajia upinzani kutoka kwa JS Saoura.

“Kagere na Bocco ni washambuliaji wazuri ambao wamekuwa wakitimiza majukumu yao ipasavyo kwa kufunga mabao, lakini niwapongeze wachezaji wote kwasababu bila wao kufanya vizuri hawa wawili wasingeweza kufunga,” alisema Aussems.

Alisema amewaandaa Bocco, Kagere kucheza soka ya kufunguka na hatacheza soka ya kujilinda kama baadhi ya wadau wanavyodhani kwa kuwa Simba itakuwa ugenini.

“Kama tulicheza mechi mbili ugenini tulishambulia tukapoteza kwa idadi kubwa ya mabao kwanini nibadilishe katika mechi hii, tutacheza kwa kushambulia kama mechi zote ambazo tumecheza tukiwa nyumbani na ugenini,” alisema Aussems.

Alisema anatambua JS Saoura itacheza soka ya kufunguka kwa kuwa itakuwa nyumbani, lakini hatakuwa na hofu nayo kwa kuwa anataka pointi tatu.

Akizungumzia namna timu yake itakavyodhibiti mashambulizi ya wapinzani wao, Aussems alisema atamkosa beki wa kati Juuko Murshid ambaye ni majeruhi.

“Kulikuwa na maelewano mazuri kati ya Wawa, Juuko na Erasto Nyoni ambaye naye atakosekana, hajapona vizuri kwa maana hiyo kuna mchezaji mwingine nimemuandaa kucheza katika eneo hili,” alisema Aussems.

Katika mechi za hivi karibuni za viporo vya Ligi Kuu Tanzania Bara, Wawa alikuwa akicheza pacha na Paul Bukaba kwenye safu ya ulinzi wa kati.

Pia alisema hatapanga kikosi kwa kukariri huku akimtolea mfano Cletous Chama au mwingine akidai lazima afuate maagizo yake kwa kile alichofundisha wakati wa mazoezi.

Simba itacheza na JS Saoura katika mazingira mazuri baada ya kushinda mechi sita mfululizo ikianza kwa kuilaza Al Ahly ya Misri bao 1-0 mechi ya Ligi ya Mabingwa kabla ya kushuka kwenye mechi za Ligi Kuu kwa kuilaza Yanga 1-0, iliichapa African Lyon 3-0 na baadaye kuifunga Azam 3-1.

Mechi nyingine, iliinyuka Lipuli 3-1 kabla ya kuilaza Stand United 3-0.

Mechi tano za mwisho kwa upande wa JS Saoura ilitoka suluhu na MO Bejaia kabla ya kuichapa Bordj Bou Arreridj mabao 2-0.

Timu hiyo iliilaza Tadjenant 2-0, iliifunga Hussein Dey bao 1-0 kabla ya kuchapwa 2-0 dhidi ya USM Alger katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu ya Algeria.

Baada ya mchezo huo Simba itabaki na mchezo mmoja dhidi ya AS Vita ya DRC.



Chanzo: mwananchi.co.tz