Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kocha Rangnick kuanza na haya matano Man U

Rangnick Vibali Kocha Rangnick kuanza na haya matano Man U

Fri, 3 Dec 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

MANCHESTER ENGLAND. BAADA ya mfululizo wa matokeo mabaya Manchester United iliamua kuachana na kocha wake Ole Gunnar Solskjaer na katika siku za hivi karibuni ilimleta Ralf Rangnick kuwa kocha wa mpito hadi msimu utakapomalizika.

Rangnick anaingia kwenye kikosi akiwa na kazi kubwa ya kufanya ili kuirudisha Man United kwenye mstari baada ya maumivu makubwa waliyopitia.

Mwanaspoti inakuletea mambo matano ambayo kocha huyu inabidi aanze nayo katika kikosi hiki.

KUONDOA MALALAMIKO YA FRED NA MCTOMINAY

Moja kati ya mambo makubwa ambayo kocha huyu anatakiwa kuyaangalia ni jinsi gani Van de Beek anaweza kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza.

Wakati wa Ole Gunnar Solskjaer kocha huyu muda mwingi alikuwa akipenda kuwatumia Fred na Scott McTominay katika eneo la kiungo cha chini jambo ambalo lilikuwa linapingwa na mashabiki na wachambuzi wengi.

Rangnick anatumia mfumo wa 4-2-2-2 ambao utahitaji uwepo wa viungo wawili wa chini ambao mmoja atakuwa na kazi ya kuhakikisha timu inasogea mbele na kumiliki sana mpira jambo ambalo Van de Beek anaweza kulifanya kwa usahihi.

KUMTUMIA SANCHO

Kwenye mechi ya kwanza tu Michael Carrick akiwa kama kocha wa muda wa Man United alimpa nafasi Jadon Sancho ambaye alionyesha kiwango bora kwa kuwasumbua sana mabeki wa Villarreal pale alipokuwa na mpira au bila ya mpira.

Wakati Solskjaer akiwa kocha mkuu, hakuwa anampa nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza lakini kwa upande wa Rangnick tayari kocha huyu anajua ubora wa Sancho kwa sababu ameshakabiliana naye mara kadhaa kwenye mechi za Bundesliga wakati anaifundisha RB Leipzig, hivyo anatakiwa kuangalia jinsi gani anaweza kumtumia ili ampe matokeo kwa sababu ni mmoja kati ya wachezaji wenye uwezo mkubwa.

NAFASI YA RONALDO

Licha ya kufunga mabao kumi msimu huu, bado kiwango cha Cristiano Ronaldo kimeonekana hakiridhishi katika baadhi ya mechi za Ligi Kuu England alizocheza, akichukua nafasi ya Edinson Cavani.

Katika mechi za hivi karibuni Ronaldo amekuwa na wakati mgumu wa kupenyezewa pasi za mwisho kwenye eneo la hatari kwenye mechi za hivi karibuni za ligi.

Kocha wa mpito aliyeteuliwa Ralf Rangnick atakuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha Ronaldo anacheza nafasi yake sahihi akiwa nyuma ya Bruno Feranandes, mwenye uwezo wa kupiga pasi ndani ya boksi.

NAFASI YA VAN DE BEEK

Kiungo huyo tangu alipotua Man United akitokea Ajax mwaka jana, hakupata nafasi nyingi za kucheza chini ya Ole Gunnar Solskjaer aliyefukuzwa kazi.

Solskjaer alimpa nafasi ya kucheza kiungo huyo wa Kimataifa wa Uholanzi kwenye mechi ya mwisho ya ligi aliyotimuliwa dhidi ya Watford na kufunga bao lakini timu hiyo ilipokea kichapo cha mabao 4-1.

Hata hivyo, hiyo itategemea na mfumo ambao Rangnick atautumia kwa ajili ya Van de Beek ili kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza.

KUWAUNGANISHA RONALDO NA BRUNO

Rangnick atamtumia zaidi Bruno kumtengenezea nafasi nyingi za kufunga wakicheza pamoja kutokana na uwezo wa kiungo huyo wa kupiga pasi za mwisho.

Ronaldo hajacheka na nyavu kwenye mechi ya ligi tangu alipofunga dhidi ya West Ham.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz