Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kocha Mbeya City ataja mbinu iliyoibana Yanga

89884 Mbeya+pic Kocha Mbeya City ataja mbinu iliyoibana Yanga

Fri, 27 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya, Dar es Salaam. Wakati Kocha wa Yanga Charles Mkwasa akitaja sababu mbili zilizochangia timu yake kupata suluhu, Amri Said ‘Stam’ wa Mbeya City amesema mbinu ya kupaki basi ilimsaidia kupata matokeo hayo.

Amri alisema alitambua Yanga ni timu bora, hivyo aliwaandaa wachezaji wake kucheza kwa kujilinda ili kuwabana wapinzani wao wasipate bao.

Alisema mbinu ya kujilinda ilichangia Yanga kucheza kwa presha hatua iliyowalazimu kutumia nafasi hiyo kufanya mashambulizi ya kushitukiza.

“Mbinu ya kujilinda na kufanya mashambulizi ya kushitukiza ilitusaidia, nilijua Yanga ni timu bora na leo (jana) imecheza vizuri kama sisi tulivyocheza, lakini sote tumegawana pointi moja moja,”alisema Amri.

Mkwasa alisema licha ya wachezaji wake kupambana kupata ushindi, lakini uwanja na uamuzi ulikuwa kikwazo kwao.

Mkwasa alisema eneo la kucheza lilijaa maji na lilikuwa likiteleza hatua iliyowapa wakati mgumu wachezaji kumiliki mpira katika kiwango bora. Pia alidai uamuzi haukuwa sahihi na wachezaji wake hakuwatendewa haki katika baadhi ya matukio hatua iliyowalazimu kumlalamikia mara kwa mara.

Hata hivyo, Mkwasa alisema anaamini mchezo ujao dhidi ya Prisons utakaochezwa Ijumaa utakuwa mzuri kwa Yanga kwa kuwa uwanja utakuwa umekauka.

Mchezo wa jana ulikuwa wa tano kwa Mkwasa tangu alipojaza nafasi ya Mwinyi Zahera. Yanga ilishinda bao 1-0 dhidi ya Ndanda, iliichapa JKT Tanzania mabao 3-2, iliifunga Alliance 2-1 kabla ya kutoka sare 1-1 na KMC.

Nahodha wa Yanga Papy Tshishimbi alifanya kazi nzuri kwa kupenyeza mipira mingi kwa David Molinga na Patrick Sibomana aliyecheza pembeni.

Molinga aliyekuwa akilindwa na idadi kubwa ya mabeki wa Mbeya City, alipambana kuifungia Yanga bao lakini juhudi zake ziligonga mwamba.

Dakika ya 18 Molinga alikaribia kufunga, lakini kiki yake ilitoka nje kabla ya kufanya hivyo dakika ya 58 baada ya kuichambua ngome ya Mbeya City.

Mabeki wa Yanga walikuwa na kazi kubwa ya kumdhibiti mshambuliaji Peter Mapunda aliyekuwa mwiba katika lango lao.

Mapunda aliyefunga mabao matano msimu huu, alikosa nafasi kadhaa za kuweka mpira wavuni ikiwemo dakika ya 72 ambapo alipiga kiki nje.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida kabla ya mechi kuanza wachezaji Mohammed Kapeta wa Mbeya City na Cleofasi Sospeter wa Yanga walitolewa kwa nguvu na polisi baada ya kugoma kutoka uwanjani baada ya timu hizo kumaliza mazoezi mapesi.

Wachezaji hao waliibua sintofahamu baada ya kila mmoja kumtegea mwenzake kutoka wakati timu hizo zikienda ndani ya nyumba vya kuvalia nguo kabla ya polisi kuingia uwanjani kuwatoa kwa nguvu.

Katika msimamo wa Ligi Kuu Yanga ipo nafasi ya tisa ikiwa na pointi 17 na Mbeya City 18 baada ya kuvuna pointi tisa.

Mbeya City:Harun Mandana, Kenneth Kunambi, Hassan Mwasapili, Samson Madeleko, Baraka Johnson, Edger Mbembela, Seleman Mangoma, George Chota, Peter Mapunda, Peter Ndagamba na Selemani Ibrahim.

Yanga:Farouk Shikhalo, Mustafa Suleman, Jafary Mohammed, Lamine Moro, Ally Mtoni, Said Juma, Deus Kaseke, Papy Tshishimbi, David Molinga, Raphael Daud na Patrick Sibomana.

Chanzo: mwananchi.co.tz