Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kocha Mbelgiji Simba kutesti mitambo kwa Wamorocco

9542 Pic+simba TanzaniaWeb

Thu, 2 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kartepe. Kocha wa Simba Patrick Aussems, anakabiliwa na mtihani wa kwanza tangu alipopewa jukumu la kuifundisha timu hiyo akichukua nafasi ya Pierre Lechantre.

Aussems leo atakuwa kwenye benchi la ufundi kwa mara ya kwanza akiingoza Simba katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Mouloudia Oujda ya Morocco.

Simba itacheza mchezo huo kwenye viwanja vya The Green Part saa 10:00 jioni, ukiwa ni wa kwanza kati ya mitatu ambayo Aussems amepanga kucheza kabla ya kurejea nchini.

Timu ya Mouloudia Oujda imepanda daraja na msimu ujao itashiriki mashindano ya Ligi Kuu Morocco, baada ya kutwaa ubingwa wa Daraja la Kwanza.

Aussems raia wa Ubelgiji, anatarajia kutumia mchezo huo kama sehemu ya mafunzo na atatumia fursa hiyo kuangalia kasoro zilizojitokeza kabla ya Simba kucheza mechi mbili zilizobaki.

Mazoezi magumu ya kujenga utimamu wa mwili aliyowapa wachezaji wake tangu walipowasili katika mji wa Kartepe, yataonekana katika mchezo wa leo kama yalikuwa na tija au vinginevyo.

Aussems anatarajiwa kutumia mfumo 4-4-2 unaotoa nafasi kwa wachezaji kucheza soka ya kushambulia na kutoa pasi za haraka.

Kocha huyo ameonekana akipenda kutumia mfumo huo au 4-3-3 tofauti na 3-5-2 uliokuwa ukitumiwa na mtangulizi wake Lechantre.

Katika mazoezi, Aussems ameonekana akitumia wachezaji wa aina tofauti akisaka kikosi cha kwanza ingawa nafasi kubwa katika safu ya ushambuliaji ni Emmanuel Okwi na Adam Salamba.

“Napenda wachezaji wangu wacheze soka ya kushambulia inayotumia zaidi nguvu, mazoezi ninayotoa yana msingi mzuri wa kujenga timu imara,” alisema Aussems.

Katika hatua nyingine, Aussems alidai hana timu anayoshabikia duniani licha ya kuzishuhudia zinapocheza.

“Sina timu ninayoshabikia duniani zaidi ni kuangalia na kuiga mbinu bora za timu inayovutia,” alisema kocha huyo.

Simba imepiga kambi mjini hapa na inatarajiwa kurejea Tanzania Agosti 5 kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, iliyopangwa kuanza Agosti 22.

Timu hiyo ndio mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Chanzo: mwananchi.co.tz