Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kocha Lechantre akusanyiwa mabegi yake

8916 Kocha+pic TZW

Tue, 12 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Aliingia mkataba wa miezi sita kuinoa Simba akichukua nafasi ya Joseph Omog.

Dar es Salaam. Wakati Simba ikiingia fainali ya SportPesa Super Cup huko Nakuru, Kenya kwa penalti na bila kufunga bao ndani ya dakika 180, kocha wake, Pierre Lechantre amezua sintofahamu baada ya kuachana na timu hiyo.

Simba imeingia fainali na kesho itacheza na Gor Mahia ya Kenya. Mshindi atakwenda London kuivaa Everton, Godson Park.

Uamuzi wa kocha huyo kutimka ni mwendelezo wa rekodi yake ya kutodumu kwenye timu kwa muda mrefu.

Siku moja baada ya kutambulishwa na Simba, Januari 19, gazeti hili lilitoa tathmini ya historia ya Lechantre kutodumu kwenye timu mbalimbali ambazo huzifundisha kutokana na kutimuliwa kwa sababu ya matokeo mabovu au migogoro na waajiri wake.

Rekodi zinaonyesha Lechantre hajawahi kufundisha zaidi ya mwaka tangu alipoondoka Cameroon 2001 baada ya kuipa ubingwa wa Mataifa ya Afrika mwaka 2000.

Lechantre ameondoka Simba baada ya mkataba wake wa miezi sita aliosaini na klabu kumalizika huku dalili za kuongezewa mkataba mpya zikionekana hazipo kwa kile kinachodaiwa kuwa klabu hiyo imekuwa ikitumia kiasi kikubwa cha fedha kumhudumia kocha huyo huku ikishindwa kuonyesha kiwango bora uwanjani kulingana na thamani na ubora wa kikosi chao.

Dalili za Lechantre kutimka zilianza kuonekana mapema tangu juzi (Alhamisi) mchana baada ya kubakia jukwaani wakati Simba ilipokuwa ikicheza na Kakamega Homeboys ya Kenya kwenye mechi ya nusu fainali ya Kombe la SportPesa Super Cup, akimuachia jukumu hilo msaidizi wake, Masoud Djuma. Kocha huyo alikuwa na mtaalamu wake wa viungo, Mohammed Aymen wakitazama mchezo huo.

Nyakati za jioni, picha za kocha huyo zilisambaa katika mitandao ya kijamii akiwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta Nairobi huku baadaye taarifa zikidai kuwa ameachana rasmi na klabu hiyo baada ya mkataba wake kumalizika.

Kocha huyo aliwasili jana jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kumalizana na Simba.

Historia ya kushangaza ya Lechantre ni pale alipoamua kuvunja mkataba wake wa kuifundisha Senegal wiki mbili baada ya kukubali kuchukua jukumu hilo mwaka 2012 kwa kile alichodai kutolipwa mshahara wake wa miezi sita ambao alitaka nchi hiyo impe kabla ya kuanza kazi ya kuinoa.

Sehemu pekee ambako Lechantre aliweka rekodi ya kufundisha kwa muda mrefu tangu alipoipa taji Cameroon mwaka 2000 ni klabu ya Al Sailiya ya Qatar aliyokaa kwa siku 242 kuanzia Novemba 1, 2003, hadi Juni 30,2004 lakini kwingineko kote amekuwa akifundisha kwa muda mfupi kisha kutimuliwa au kuingia mitini.

Mkufunzi wa makocha na mchambuzi wa soka, Dokta Mshindo Msolla alitaja sababu mbili ambazo anahisi zimesababisha Lechantre kuachana na Simba.

“Hata mimi nimeziona hizo taarifa lakini kama ni kweli basi naamini tatizo la kwanza ni kutokuwa na umakini katika utafutaji wa hawa makocha. Klabu zetu hasa hizo Simba na Yanga zimekuwa haziwatumii watu sahihi katika kusaka makocha hivyo wanaweza kumpata mtu ambaye hawafahamu hata rekodi yake katika ufundishaji.

Unaweza kuona kocha ana wasifu mzuri lakini ana rekodi ya kutodumu kwenye timu sasa ukajikuta unashawishika kumchukua mwisho wa siku ndio yakatokea kama haya ya Lechantre.

Hata hivyo, alipotafutwa Kaimu Rais wa Simba, Abdallah Salim ‘TryAgain’ kuzungumzia mustakabali wa kocha huyo baada ya kutoka naye Nakuru, simu yake ilikuwa ikiita bila majibu.

Chanzo: mwananchi.co.tz