Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kocha Gor Mahia aipa Simba SC masharti haya

Tue, 12 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Nakuru. Wakati mkataba wa Mfaransa Pierre Lechantre ukiwa njia panda, kocha wa Gor Mahia, Dylan Kerr amesisitiza yuko tayari kurejea Simba, lakini ametoa masharti magumu.

Akizungumza mjini hapa jana, Kerr alisema amefurahi kuifunga Simba katika mchezo wa fainali ya michuano ya SportPesa Super Cup.

Gor Mahia ilishinda mabao 2-0, katika mchezo wa fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa Afraha, Nakuru, jana.

Kerr alisema kuwa kipigo dhidi ya Simba ni salamu kwa mabosi wa klabu hiyo ambao baadhi yao walimuona mzigo na kupendekeza afukuzwe.

Kocha huyo aliyetimuliwa Simba Januari 2016, alisema baada ya kuichapa Simba, yupo tayari kurejea klabuni hapo, lakini kwa masharti magumu.

Kerr aliyepata mafanikio nchini Vietnam alisema anafahamu Simba ipo chini ya Rais mwingine (Salim Abdallah ‘Try Again’) na uwekezaji wa Mohammed Dewji ‘MO’, hivyo hatakuwa na tatizo kufanya nao kazi.

Alisema ili aweze kurejea Simba lazima baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji waondolewe kwa madai walikuwa sababu kubwa kwake kutimuliwa miaka miwili iliyopita.

“Kuna mjumbe mmoja alisema hajawahi kuona Simba mbovu kama yangu. Nashukuru amekuja hapa Kenya na ameona uwezo wa timu yangu ya Gor Mahia.

“Kama walisema nilikuwa mbovu Simba, imekuwaje sasa nina timu nzuri, timu inayofanya vizuri kwenye mashindano yote. Narudia tena, Simba walikuwa na haraka kunitimua.

“Nimemuona Rais wa sasa wa timu hiyo, ni mtu mwema, nasikia pia wana mwekezaji mkubwa. Ni jambo jema lakini kama baadhi ya wajumbe wa bodi hawataondolewa, siwezi kurudi,” alisema Kerr ambaye alishtushwa na taarifa za kutimuliwa kwa Lechantre ambaye ameipa Simba ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara hivi karibuni.

Simba ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliomalizika baada ya kuukosa kwa miaka mitano.

Awali, muda mfupi kabla ya kuondoka nchini, Kerr alipozungumza na gazeti alisema anaondoka Simba akiwa bado ana mapenzi na klabu hiyo.

Kocha huyo raia wa Uingereza alidai kuwa ataikumbuka Simba kwa kutomaliza programu yake ya kazi, kupendwa na mashabiki wa klabu hiyo na Watanzania wanavyopenda soka.

Chanzo: mwananchi.co.tz