Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Klabu zabadili msimamo mwenyeji kuchukua mapato

13967 Klabu+pic TanzaniaWeb

Mon, 27 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Sasa zataka kutengua uamuzi wa awali ili mapato yagawanywe sawa .

Dar es Salaam. Wakati Ligi Kuu Bara ikiingia raundi ya pili, timu mbalimbali za ligi hiyo zimeendelea kulia kwa ligi hiyo kukosa mdhamini na ukosefu wa mapato ya mlangoni.

Baadhi ya klabu za Ligi Kuu Bara tayari zimeanza kuonja joto ya jiwe na sasa zinataka uamuzi waliofikia awali wa mwenyeji kuchukua mapato yote utenguliwe.

Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni kutokana na kukosekana mdhamini wa ligi hiyo na baadhi ya klabu kukosa mashabiki kuwapa mapato.

Awali kabla ya kuanza ligi hiyo Agosti 22, klabu zilikubaliana utaratibu wa kuchukua mapato, lakini sasa inaonekana hali inakuwa ngumu. Bodi ya Ligi ilipitisha mapendekezo ya klabu kuwa timu mwenyeji ichukue mapato yote katika mchezo husika tofauti na zamani jambo ambalo limeonekana kuziumiza klabu nyingi hasa ndogo.

Ukiziondoa Simba, Yanga, timu nyingi zimekuwa na mashabiki wachache wanaoingia viwanjani hivyo kuzikosesha mapato ya mlangoni.

Baadhi ya timu zimeshauri utaratibu wa zamani wa klabu kugawana mapato urejeshwe ili kuziokoa na janga hilo hasa katika pande wa usafiri na kambi.

Wakizungumza na Mwananchi jana, Msemaji wa JKT Ruvu, Koplo Jamila Mutabazi ameshauri utaratibu wa zamani wa timu kugawana mapato urejeshwe ili kuzisaidia klabu nyingine hasa ndogo.

“Katika uhalisia hiyo ni changamoto kubwa kwa klabu ndogo ambazo hazijafikia hatua ya kuwa na mashabiki wengi kama ilivyo kwa Simba na Yanga.

“Mapato yote kuchukua timu mwenyeji na wageni kutopata ni changamoto katika suala la kiuchumi hasa wakati huu ambao ligi haina mdhamini. Uendeshaji wa timu ni gharama hivyo nashauri utaratibu wa zamani ungerejea ili kuzisaidia klabu ndogo,” alisema Jamila.

Msemaji wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru alisema Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi zinatakiwa kufanya hima kurejesha utaratibu wa zamani wa timu zote kugawana mapato katika mechi la sivyo kuna timu zitashindwa kufika vituoni kwa wakati.

“Mtibwa hatuna shida sana kwani inaendeshwa na kampuni lakini hizo timu nyingine hasa za mikoani zitapata taabu sana.

“Bora utaratibu urudishwe kwa timu kugawana mapato nusu kwa nusu kila mechi kuliko sasa mwenyeji anachukua mapato yote, yaani mtu unasafiri kwenda mkoani unarejea patupu huwezi hata kupata hela ya mafuta.

“Simba na Yanga ndio zitanufaika na hili, wanaoendesha ligi wanatakiwa kuliangalia hili kwa haraka ama kutafuta udhamini au kurejesha utaratibu wa zamani wa kugawana mapato.”

Katibu mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe alisema suala la mapato ni changamoto kubwa kwa timu nyingi hasa ndogo lakini tayari uamuzi umeshafanyika hivyo hawawezi kurudi nyuma.

“Ligi kukosa mdhambini ni changamoto kubwa na hata hii ya timu mwenyeji kuchukua mapato yote inaweza kuwa nzuri kwa upande mmmoja lakini mbaya kwa upande mwingine hasa kwa timu zisizo na mashabiki wengi.

“Ninaweza kusema tubadilishe utaratibu na kurejesha mfumo wa zamani wa timu kugawana mapato ya mechi husika lakini kwa sasa itakuwa ngumu kwani tayari mechi za raundi ya kwanza zimeshachezwa na timu zishachukua chao hivyo ukisema urudi kama zamani utakuwa hujazitendea haki timu nyingine.

Hata hivyo, ni mzunguko mmoja umechezwa na jana zilichezwa mechi mbili na nyingine zinaendelea leo.

“Muhimu ni kuhakikisha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linapambana kutafuta mdhamini mkuu wa ligi ili kuziokoa timu shiriki,” alisema Kimbe.

Katibu mkuu wa Prisons, Havintishi Abdallah alisema hilo ni tatizo kubwa na bora utaratibu wa zamani wa kugawana mapato ukarejeshwa.

“Kukosa mdhamini mkuu katika ligi ni tatizo kubwa tena kubwa sana, hapa ndio kwanza mechi ya kwanza zikifika tano na kuendelea hali itakuwa mbaya zaidi na zitakazofanya vizuri ni timu kubwa tu ambazo zinawezakujiendesha.

“Unakwenda ugenini unatumia gharama kubwa na unarudi bila kupata kitu (mapato), ninafikiri utaratibu wa zamani wa timu kugawana mapato katika mechi ungerejeshwa tu hata kama nyingine ni ndogo, lakini zinasaidia ili kuziokoa timu nyingi,” alisema Havintishi.

Katibu wa Ruvu Shooting, Suleman Mohammed alisema utaratibu wa kukusanya mapato kwa mwenyeji unaweza kuzinufaisha zaidi timu kubwa kuliko ndogo ambazo zimekuwa zikisuasua.

“Hakuna mwarobaini wa kutatua hili zaidi ya kupatikana kwa mdhamini mkuu kwa sababu hata mapato ya viwanjani hayawezi kukidhi mahitaji ya timu, kadri udhamini unavyochelewa ndivyo hali itakavyozidi kuwa mbaya,” alisema Mohammed.

Mwenyekiti wa Mbao FC, Solly Njashi alisema TFF, inatakiwa kuendelea kupambana ili kuhakikisha anapatikana mdhamini wa Ligi Kuu Bara.

“Kama mazingira magumu tumezoea na hata ukisema turudi kwenye ule utaratibu wa mwanzo wa kugawana mapato ya uwanjani bado mapato hayo hayawezi kuifanya timu ijiendesha,” alisema mwenyekiti huyo.

Meneja wa Biashara United ya Mara, Aman Josiah alisema hiki ni kipindi kigumu hasa kwa timu zenye uchumi wa kati na chini kutokana na kutokuwa na vyanzo vingi vya mapato.

“Udhamini umebeba ligi nzima, bila udhamini hakuna ligi. Huo ni ukweli mtupu na hata upangwaji wa matokeo unaweza ukatokea kwa wepesi kutona na njaa inayosababishwa na ukosefu wa mdhamini mkuu, lakini tunaiombea TFF ili itukomboe,” alisema Aman.

Mkurugenzi wa Alliance, James Bwire alisema wameanza kuweka mikakati ambayo wanaamini itawakwamua kwenye kipindi hiki ambacho TFF inaendelea kutafuta madhamini mkuu wa ligi.

“Mapato ya viwanjani si kitu kikubwa tunatakiwa kubadilika kwa kuanza kuwa na mawazo ya kutotegemea udhamini wa ligi, udhamini huo iwe ni ziada tu.

“Itatuchukua muda kuhama huko ili kama tukifanikiwa tunaweza kuwa na ligi bora yenye ushindani kutokana na klabu mbalimbali kuwa na uwezo binafsi wa kujiendesha,” alisema Mkurugenzi huyo.

Meneja wa Azam, Philipo Alando alisema jambo hilo ni changamoto kubwa kwa timu zisizo na mashabiki lakini ni ngumu kubadilisha lolote kwa sasa kwani tayari uamuzi ulishafanyika kabla ya ligi.

“Timu nyingi hasa ndogo zitaathirika kwenye mapato kwani hazina mashabiki wengi na hata sisi Azam hilo linatukuta kwani hatuna idadi kubwa ya mashabiki lakini tayari maamuzi yalishafanyika ni ngumu kuyabadilisha kwa sasa kwani tayari ligi imeanza. Kinachotakiwa ni wadhamini kujitokeza kudhamini ligi,” alisema Alando.

TFF watoa neno

Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau ameonekana kushangazwa na madai hayo akisema kuwa klabu hizo ndizo zilizopendekeza hilo.

“Tulikaa nao chini na yakapitishwa mapendekezo yao kwa hiyo unaponieleza hilo nashindwa kuelewa kwa sababu haukuwa uamuzi wetu, waliamua wenyewe na Bodi ya Ligi ikalipa baraka,” alisema Kidau.

Wakati huo huo, Ligi Kuu Bara inaendelea leo kwa JKT Tanzania kucheza dhidi ya Lipuli wakati Ruvu Shooting itaikaribisha KMC kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani, Stand United itakuwa na kibarua mbele ya Mbao FC.

Michezo mingine mitatu ambayo inatarajiwa kuchezwa kesho ni Azam ambao watatupa karata yao ya pili dhidi ya Ndanda FC wakati Alliance itacheza dhidi ya African Lyon huku Simba wakikipiga na Mbeya City kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Chanzo: mwananchi.co.tz