Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kiwango cha Serengeti Boys chashtua, wapigwa 5-0

45804 Pic+serengeti Kiwango cha Serengeti Boys chashtua, wapigwa 5-0

Mon, 11 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mashirika. Kiwango kilichoonyeshwa na timu ya taifa ya Tanzania kwa vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys kwenye michuano ya Uefa Assist, kimeshtua mashabiki wa soka ikiwa ni mwenyeji wa Fainali za Afcon kwa vijana zinazoanza Aprili 14 hadi 28 mwaka huu.

Serengeti Boys ilimaliza mechi zake tatu kwa kufungwa mabao 5-0 na Uturiki ikiwa imeruhusu mabao nane huku ikifunga matatu.

Michuano ya Uturuki imeandaliwa na Uefa kwa ajili ya timu za vijana zinazojiandaa na mashindano mbalimbali. Jumla ya timu 12 zilishiriki michuano hiyo.

Akizungumzia mashindano hayo, Mkuu wa Vyama vya Soka na Uhusiano wa Kimataifa wa Uefa, Eva Pasquier, alisema: “Huu ni mpango wa Uefa Assist wenye lengo la kugawana uzoefu kwa timu wanachama wa Uefa na marafiki wa Uefa.

Mataifa yaliyoshiriki michuano hiyo ni; Cameroon, Uganda, Morocco na Belarus zilizokuwa Kundi B wakati Kundi C lilikuwa na timu za Senegal, Nigeria, Angola na Montenegro.

Tanzania ilianza kwa kufungwa bao 1-0 na Guinea kabla ya kuilaza kwa mbinde Australia mabao 3-2 na mchezo wa mwisho kuambulia kipigo kitakatifu cha Uturuki.

Katika mchezo wa jana, wachezaji wa Serengeti Boys walionekana kukosa mfumo mmoja wa kucheza kitimu, wachezaji kutofahamiana kwa nafasi zao uwanjani lakini pia kushindwa kutengeneza nafasi za kupata mabao. Washambuliaji wa Serengeti Boys wakiongozwa na Kelvin John walionekana kushindwa kufanya uamuzi hasa wanapolifikia lango la wapinzani wao na kujikuta wakipiga chenga zisizo na faida na mwisho kunyang’anywa mipira.

Pia wachezaji walionekana kukosa stamina kwani hata mashuti waliyopiga golini yalionekana hafifu na mengi yaliishia mikononi mwa kipa wa Uturuki.

Mchambuzi wa masuala ya soka, Ally Mayay alisema tatizo kubwa lililopo ndani ya Serengeti Boys na ambalo linatakiwa kufanyiwa kazi haraka ni kukosa umakini.

“Ukiangalia wale vijana wanafanya makosa mengi, eneo lingine ni mabeki. Wengi ni wafupi sasa ukikutana na timu ambazo zina washambuliaji wenye maumbo makubwa inaweza kuwa tatizo zaidi.”

Katibu wa zamani wa (TFF), Angetile Osiah alisema wachezaji wa Serengeti Boys wanakosa utimamu wa mechi.

“Uturuki walionekana kucheza soka la kufundishwa, wanacheza kwa nidhamu ya mpira, na mbinu tofauti na sisi. Hata jinsi wanavyotafuta mpira wakipokonywa, wanapambana kwa ushirikiano sana.”

“Wa kwetu wanakosa utimamu wa mechi yaani hawako fiti kwa sababu hawapati mechi nyingi za kuwapa mazoezi. Nafikiri kama wangekuwa wanacheza katika klabu za ligi wangepata uzoefu kwani wangecheza mechi nyingi.

“Ukiangalia kwa sasa hii timu inasubiri mpaka iwe na mashindano ndio waingie kambini na kuanza mazoezi lakini nashauri kungewekwa kanuni labda mfano ligi daraja la pili iwe kwa ajili ya vijana tu yaani timu ziwe zinasajili wachezaji asilimia kubwa vijana chini ya miaka 17 na wale wakubwa wawe watatu wa wanne, ili kukuza soka la vijana”alisema Angetile.



Chanzo: mwananchi.co.tz