Bingwa wa London Marathon, Kelvin Kiptum, aliipa kisogo Mashindano ya Riadha Duniani yaliyofanyika Budapest nchini Hungary na Berlin Marathon nchini Ujerumani ili kuelekeza nguvu zake kwenye mbio za Chicago Marathon.
Na wikendi hii, Jumapili 8, macho yatamulikwa kwa Kiptum akisaka ubingwa wa Chicago Marathon nchini Marekani ambayo ni moja ya marathon sita maarufu duniani huku funga dimba ikiwa ni mwezi ujao kwenye mbio za New York City Marathon, Marekani.
Kiptum anatabiriwa kuendeleza pale alipoachia gwiji wa mbio za kilomita 42, Eliud Kipchoge, wiki mbili zilizopita kwenye Berlin Marathon, mashindano ambayo wengi walidhani wangeshuhudia wawili hao wakitunishana misuli.
Hata hivyo, kiu ya Wakenya ni kuona moja wao au ikiwezekana mwanariadha yoyote raia wa Kenya akivunja rekodi ya dunia inayokaribia kugonga chini ya saa mbili.
Kipchoge alikuwa amelenga kuivunja rekodi yake ya dunia ya saa mbili, dakika moja na sekunde tisa lakini akamaliza kwa saa 2:02:42 na kuweka rekodi ya kuwa mwanariadha wa kwanza kushinda mbio za Berlin Marathon mara tano.
Sasa ni zamu ya Kiptum ambaye ni mtu wa pili kukimbia kwa kasi mbio za marathon akikosa sekunde 17 tu kuvunja rekodi ya dunia iliyowekwa na Kipchoge kwenye mbio za Berlin Marathon mwaka jana.
Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 23 akitumia ukurasa wake wa Facebook alitangaza ushiriki wake katika mbio za Chicago Marathon akiwaambia mafans wake wajiandae kwa mambo mazuri.
“Naelekea Bank of America Chicago Marathon 2023 hivyo jiandaeni kwa shoo tamu,” huu ndiyo ujumbe aliyoposti Kiptum.
Rekodi tano za dunia zimevunjwa Chicago Marathon ambapo tatu ni upande wa wanaume na zingine mbili kwa wanawake, mara ya mwisho ikiwa ni mwaka 2013 na Dennis Kimetto kwa muda wa saa 2:03:45 ambapo inabaki rekodi ya Chicago.
Mara ya kwanza rekodi ya dunia kuvunjwa kwenye Chicago Marathon ilikua 1984 na Steve Jones raia wa Wales kwa muda wa saa 2:08:05 na tena mwaka 1999 na Khalid Khannouchi raia wa Marekani ila mzaliwa wa Morocco aliyetimka kwa muda wa saa 2:05:42 kabla ya rekodi iliyowekwa na Kimetto.
Na kwa upande wa wanawake, Catherine Ndereba aliweka rekodi ya dunia Chicago Marathon mwaka 2001 kwa muda wa saa 2:18:47 na ikavunjwa mwaka moja baadaye na Muingereza Paula Radcliffe akiweka muda wa saa 2:17:18.
Kiptum atakuwa analenga kuwa mwanariadha wa nne mwanamume anayeshiriki Chicago Marathon kuvunja rekodi ya dunia ikiwemo kushinda marathon yake ya tatu.
Alishiriki mbio zake za kwanza mwaka jana nchini Hispania kwenye Valencia Marathon na kuwa mtu wa tatu kukimbia chini ya saa mbili na dakika mbili akiibuka mshindi kwa kutumia muda wa saa 2:01:53.
Kiptum anatarajia kupata upinzani mkali kutoka kwa bingwa mtetezi wa Chicago Marathon Benson Kipruto aliyejiwekea muda bora wa saa 2:04:24 akishinda mbio hizo na alimaliza nafasi ya tatu mbio za Boston Marathon 2022 akitumia muda wa saa 2:07:27 na pia nafasi hiyo hiyo katika mbio hizo hizo mwaka uliyofuata kwa muda wa saa 2:06:06.
Wengine watakaomtoa jasho Kiptum ni John Korir ambaye muda wake bora marathon ni saa 2:05:01 na Daniel Mateiko na Wesley Kiptoo wanaoshiriki mbio za marathon kwa mara ya kwanza.
Pia wamo Bashir Abdi mzaliwa wa Somalia mwenye uraia wa Ubelgiji aliyeshinda medali ya dhahabu Michezo ya Olimpiki Tokyo, Japan mwaka 2020, Galen Rupp raia wa Marekani mshindi wa medali ya fedha mbio za mita 10,000 Michezo ya Olimpiki London mwaka 2012 na medali ya shaba mbio za marathon Olimpiki za Rio nchini Brazil mwaka 2016 na bingwa wa Chicago Marathon 2021, Muethiopia Seifu Tura, aliyemaliza nyuma ya Kipruto mwaka jana.