Eliud Kipchoge amepewa tuzo ya ufahari kufuatia kiwango bora alichokionesha wakati wa michezo ya Olimpiki iliyofanyika Tokyo nchini Japan.
Gwiji huyo wa riadha alivumilia hali mbaya ya hewa katika mji wa Sapporo na kuibuka na ushindi katika mbio za wanaume.
Kipchonge mwenye umri wa miaka 36, aliudhihirishia ulimwengu kwa nini yeye ni bora baada ya kuchukua medali ya dhahabu katika mbio za marathoni.
Dunia ilimshuhudia Kipchoge akifanikiwa kutetea medali yake ya Olimpiki, katika fainali zilizofanyika Tokyo, huku akiwa ni mwanariadha wa tatu katika historia kuweza kufanya hivyo.
Kiwango cha Kipchoge hatimaye kimemuwezesha kunyakua tuzo hiyo ya mwanamichezo borra wa michuano ya Olimpiki akiwashinda wanamichezo wengine nane waliokuwa wakipambanishwa nae.
Mwanariadha mwingine kutoka Uganda, Joshua Cheptegei ambae nae alishinda medali ya dhahabu katika michezo ya Olimpiki mwaka huu alikuwa ni miongoni mwa washindani wake
Akionesha hisia zake baada ya kushinda tuzo hiyo Kipchoge ameona ni heshima kutambuliwa kama mwanamichezo bora wa michuano hiyo.
"Ni heshima kwangu kushinda tuzo hii, kwa viwango bora vilivyooneshwa na wanamichezo katika fainali zile, ninajisikia fahari kutunukiwa tuzo hii kama mshindi" ameandika Kipchoge katika mtandao wake wa Twitter
"Ahsanteni wote kwa ushirikiano wenu" ameongeza Kipchoge