NYOTA wa wanne wa Simba ambao ni Jonas Mkude, Cletous Chama, Erasto Nyoni na Gadiel Michael waliokuwa na msala wa makosa ya utovu wa nidhamu wamejisalimisha kwa vigogo wa klabu hiyo na kilichobaki sasa ni kupigwa panga kwenye fedha zao kama adhabu ya makosa yao.
Wachezaji hao walizua mjadala baada ya kuitwa Taifa Stars wakiwa na makosa klabuni, wanadaiwa kujitetea kwenye Kamati ya Maadili ambayo iliwasilisha taarifa ya kila kilichofanyika kwa ofisa mtendaji mkuu wa klabu hiyo, Senzo Mazingiza ambaye anasikiliziwa kutoa hukumu gani.
Hata hivyo, Senzo aliliambia Mwanaspoti jana kuwa baada ya kuwasimamisha wachezaji hao aliwataka waandike barua ya kujieleza waliyotakiwa waipeleke katika Kamati ya Maadili aliyoiteua.
“Baada ya hapo waliruhusiwa kufanya shughuli zote za klabu kama hivi sasa unawaona mpaka mechi wamecheza, lakini watakwenda kukutana na adhabu za ndani kwa ndani kutokana na utetezi wao ambavyo walieleza,” alisema Senzo bila kuufafanua utetezi ama adhabu hiyo.
“Tumeamua kulifanya hilo ili kutengeneza nidhamu ndani ya timu kuanzia kwa wachezaji bila ya kujali ukubwa wa majina yao mpaka katika maeneo mengine ili timu yote kuwa katika nidhamu sawa jambo ambalo litatusaidia kufikisha malengo yetu,” alisema na kuongeza:
“Hivyo Mkude, Chama, Nyoni na Michael wataendelea kufanya shughuli za klabu kama kawaida ila hawatasimamishwa kama wengi wanavyodhani, bali adhabu zitakuwa ni zile za ndani lakini mhusika atahisi maumivu ambayo hatakubali kufanya tena jambo kama hilo.”
Pia Soma
- Magori: Sababu hizi zilitung'oa mabingwa
- Pyramids inafungika dakika hizi
- Scholes ataja magonjwa matatu Man United