Kampala, Uganda. Timu ya taifa ya Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars' leo asubuhi imefanya mazoezi katika mvua kujiandaa na mechi yake dhidi ya Zanzibar kesho Jumanne katika mashindano ya Chalenji yanayoendelea nchini Uganda.
Mazoezi hayo yalifanyika kwenye Uwanja wa KCCA uliopo Lugogo jijini Kampala itakapofanyika mechi ya kesho itachezwa kuanzia saa 10 jioni.
Mvua hiyo ambayo ilianza kunyesha nyakati za asubuhi, ilikuta Stars ikiwa imeshaanza programu ya mazoezi ambayo iliendelea kufanywa hadi pale ilipomalizika ndipo wachezaji wakatoka uwanjani huku wakiiacha ikiendelea kunyesha.
Katika programu hiyo ya asubuhi, kocha Juma Mgunda alitenga makundi mawili ambapo la kwanza lilikuwa ni la wachezaji waliocheza dakika zote za mechi ya jana ambayo Kilimanjaro Stars ilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Kenya.
Kundi la pili ni wachezaji ambao hawakutumika na wale ambao hawakucheza kwa dakika zote 90 za mchezo.
Wachezaji wa kundi la kwanza walifanya mazoezi mepesi mafupi na kisha kupewa nafasi ya kupumzika na huku kundi la pili likifanyishwa mazoezi ya viungo, kukimbia na kuchezea mpira kwa muda zaidi ya ule wa wenzao.
Kocha Mgunda alisema mazoezi hayo yalikuwa maalum kwa ajili ya wachezaji kujiweka sawa kabla ya mchezo wa kesho.
"Kubwa tumefanya mazoezi ya kuwaimarisha 'recovery' wale waliocheza jana na ambao hawakucheza maana yake hawakufanya mazoezi jana hivyo tumewapa mazoezi yao ili wawe katika kiwango sawa na wale waliocheza," alisema Mgunda