Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kilichomponza Zahera Yanga hiki hapa

82387 Zahera+pic Kilichomponza Zahera Yanga hiki hapa

Fri, 1 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kipigo cha mabao 2-1 ilichopata Yanga dhidi ya Pyramids ya Misri kimetajwa si sababu ya kuwepo shinikizo la kutaka Kocha Mwinyi Zahera kung’olewa katika kikosi hicho.

Matokeo hayo yameiweka Yanga katika nafasi finyu ya kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika na sasa inatakiwa kushinda kuanzia mabao 2-0 ili kusonga mbele.

Wakizungumza na gazeti hili jana, makocha na wachambuzi nchini wamedai kabla ya mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Jumapili hakukuwa na dalili nzuri kwa Zahera.

Kocha Joseph Kanakamfumu alisema kipigo dhidi ya Pyramids ni kama hitimisho la udhaifu wa Zahera kwa kuwa alitakiwa kuwajibishwa mapema.

“Msimu huu ndiyo timu yake iwe hakusajili wachezaji wote au vipi lakini kazi ya kocha ni kuwaunganisha wacheze mpira Wa ushindani.

“Moja ya udhaifu wa Zahera ni kutojua kupanga kikosi kutokana na mechi husika,” alisema Kanakamfumu. Mchambuzi Alex Kashasha alisema kabla hata ya kuvaana na Pyramids, Yanga ilikuwa na udhaifu.

“Kinachotokea kwa wapenzi wa Yanga ni sahihi timu haionyeshi kuimarika. Kufungwa sio shida ila tatizo linakuja timu inapokuwa haionyeshi kuimarika haina muunganiko mzuri.

“Sasa kama inafika muda wa miezi sita bado timu haipo sawa usitegemee kufanya vizuri.

“Uwezo wa mchezaji mmoja mmoja umepungua hapa mwalimu hawezi kuepuka lawama, ukifuatilia kwa undani utakubaliana na mimi chanzo cha matatizo ya Yanga ni pale walipomtimua kocha Hans van der Pluijm,” alisema Kashasha.

Kocha Boniface Pawasa alisema usajili uliofanywa na Yanga msimu huu ndio ulianza kumkaanga Zahera.

“Mwalimu anapaswa kukubali kuvaa joho la lawama ukiangalia usajili wa msimu huu kwa zaidi ya asilimia 68 umetokana na mapendekezo ya kocha lakini hadi sasa ameshindwa kutengeneza kikosi cha kwanza na sijawahi kuona timu imefanikiwa bila kikosi cha kwanza.

Beki huyo wa zamani wa Simba alisema Yanga wanapaswa kumpa muda Zahera kujadili namna ya kuboresha kikosi na si kumwondoa katika benchi la ufundi.

Naye Bakari Malima alisema Zahera anatakiwa kupewa muda kwa kuwa hapaswi kuhukumiwa kwa matokeo dhidi ya Pyramids.

Yanga ina kibarua cha kufanyia kazi mbinu zake, kuwajenga wachezaji kisaikolojia na kuhakikisha wanakuwa fiti kukabiliana vyema na ikibidi kuibuka na ushindi wa ugenini.

Hata kabla ya mchezo Yanga ilionekana kuwa na shida katika mbinu na upangaji wa kikosi jambo ambalo limekuwa likichangia ishindwe kuonyesha kiwango bora msimu huu.

Kuwapanga wachezaji katika nafasi ambazo sio sahihi, imani kwa wachezaji ambao hawatoi mchango mkubwa kwenye kikosi na kutowapa nafasi nyota wanaonekana kuwa na kiwango bora ni miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakiigharimu timu hiyo.

Wakati huo huo, Yanga inatarajiwa kuondoka leo kwenda Misri kuikabili Pyramids katika mchezo wa marudiano utakaochezwa Novemba 3.

Chanzo: mwananchi.co.tz