Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kilichoiponza Yanga hiki hapa

56046 Pic+yanga

Tue, 7 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam.Udhaifu wa mabeki na papara za washambuliaji wa Yanga katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Azam Sports Federation dhidi ya Lipuli ya Iringa, vimeiweka timu hiyo katika nafasi ndogo ya kucheza michuano ya kimataifa msimu ujao.

Makosa hayo ya kiufundi ambayo kwa kiasi kikubwa yalitumiwa vyema na Lipuli waliokuwa wenyeji wa mchezo, jana yaliigharimu Yanga na kujikuta ikichapwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Samora, Iringa.

Yanga imetupwa nje ya mashindano hayo jambo ambalo linawalazimisha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara ili kurudi kwenye michuano ya kimataifa msimu ujao.

Katika mchezo wa jana, mabeki wa Yanga, walifanya kosa kumuacha Paul Nonga apige shuti lililozaa bao la kuongoza dakika ya 28 akiunganisha mpira uliopanguliwa na kipa Klausi Kindoki kutokana na kiki ya Jimmyshoji Mwasondole .

Mchezaji Daruwesh Saliboko alifunga bao la pili dakika kumi baadaye akimalizia shambulizi la piga nikupige langoni mwa Yanga, baada ya mabeki kuzembea kuokoa hatari iliyoelekezwa langoni mwao.

Mbali na uzembe uliosababisha mabao hayo mawili, ukuta wa Yanga uliokuwa na mabeki Haji Mwinyi, Andrew Vincent ‘Dante’, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na Paul Godfrey ulikuwa ulifanya makosa ya mara kwa mara ambayo kama si uhodari wa Kindoki kuokoa na kukosa umakini kwa safu ya ushambuliaji ya Lipuli, wangeweza kufungwa zaidi ya mabao hayo.

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera alimtoa Ibrahim Ajibu na kumuingiza Juma Abdul kucheza nafasi ya beki wa kulia na Godfrey alisogezwa winga wa kulia. Pia aliwatoa Mwinyi na Mohammed Issa ‘Banka’ ambao nafasi zao zilichukuliwa na Amissi Tambwe na Kelvin Yondani.

Dakika ya 68 hadi 83 Yanga ilipata nafasi ambazo Amissi Tambwe, Ibrahim Ajibu, Mrisho Ngassa na Heritier Makambo walishindwa kuzitumia kufunga mabao.

Lipuli imekata tiketi ya kucheza fainali ya mashindano hayo itakayofanyika kwenye Uwanja wa Ilulu mkoani Lindi ambako itaumana na Azam FC Juni 2 na mshindi atapata tiketi ya kuiwakilisha Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.

Hata hivyo licha ya kuongoza msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 80 baada ya kucheza mechi 34, wanakabiliwa na presha kubwa kutoka kwa Simba wanaoshika nafasi ya pili wakiwa na pointi 78 huku wakiwa wamecheza michezo 30 tu.

Yanga itapaswa kuomba Simba wafanye vibaya kwenye mechi zote zilizosalia ili watwae ubingwa kwani watani wao wa jadi wakipata ushindi kwenye mechi tano tu kati ya nane walizobakiza, watafikisha pointi 83 abazo hazitofikiwa na Yanga hata ikipata ushindi kwenye mechi zake zote nne zilizobaki kabla ya ligi kumalizika.

Kikosi cha Yanga ni Klaus Kindoki, Paul Godfrey, Mwinyi Haji, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Andrew Vicent ‘Dante’, Faisal Salum ‘Fei Toto’, Mrisho Ngassa, Mohamed Issa, Heritier Makambo, Pappy Tshishimbi na Ibrahim Ajib.

Kikosi cha lipuli ni Yusuph Mohamed, William Gallas, Paul Ngelema, Ally Sonso, Haruna Shamte, Fredy Tangalu, Miraji Athuman, Jimmyshoji Mwasondole, Paul Nonga, Daruwesh Saliboko na Zawadi Mauya.



Chanzo: mwananchi.co.tz