Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kili Stars, Uganda mechi ya kisasi

88906 Uganda+pic Kili Stars, Uganda mechi ya kisasi

Wed, 18 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kampala, Uganda. Udhaifu wa mabeki Uganda unaweza kuwa msaada kwa timu ya Taifa ya Tanzania Bara, ‘Kilimanjaro Stars’ kupata ushindi katika mchezo wa nusu fainali wa mashindano ya Kombe la Chalenji utakaochezwa leo.

Mabeki wa Uganda wamekuwa wakifanya makosa mara kwa mara ya kuruhusu washambuliaji wa timu pinzani kufikia lango lao ambayo yamekuwa yakichangiwa na mawasiliano duni na kutegeana baina yao.

Ingawa timu hiyo inaonekana tishio, changamoto hiyo inaonekana kushindwa kufanyiwa kazi na benchi lake la ufundi na huenda ikageuka neema kwa Kilimanjaro Stars zitakapokutana katika mchezo wa pili wa nusu fainali utakaochezwa Uwanja wa KCCA saa 10 jioni.

Awali ratiba ilionyesha timu hizo zingecheza mechi ya kwanza saa 7.30 mchana lakini juzi ilibadilishwa na kuiweka iwe ya pili ikitanguliwa na ile itakayozikutanisha Eritrea na Kenya.

Makosa hayo yameifanya Uganda kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili katika mechi ya kwanza ya hatua ya makundi dhidi ya Burundi ambayo ilishinda mabao 2-1 na mechi ya mwisho ilipocheza na Djibout waliyoshinda 4-1.

Hata hivyo, uimara wa safu ya ushambuliaji na kiungo wa Uganda unapaswa kuifanya Kilimanjaro Stars kuingia na tahadhari ya hali ya juu katika mechi hiyo.

Safu ya kiungo inayoongozwa na Muzamiru Mutyaba, Bright Anukani imeleta muunganiko mzuri wa kitimu ambao umechangia Uganda kutawala mchezo, kutengeneza nafasi na kufunga idadi kubwa ya mabao kulinganisha na timu nyingine ambazo zimeshiriki mashindano hayo.

Uganda imefunga mabao 10 katika mechi nne huku Anukani na Allan Okello kila mmoja akifunga mawili yanayowafanya kuwa vinara katika mbio za kuwania ufungaji bora.

Okello anayecheza KCCA ya Uganda anapaswa kuchungwa kutokana na ujanja wake wa kufunga, uwezo wa kutengeneza nafasi na kuwatoka mabeki wa timu pinzani.

Kilimanjaro Stars kwa upande wake ina maeneo ambayo yanaweza kuibeba na yale ambayo inapaswa kuyafanyia kazi ili ifanye vizuri.

Udhaifu wake upo katika safu ya ushambuliaji ambayo imekuwa ikipoteza nafasi ambazo inatengeneza na pia eneo la kiungo halijatengeneza muunganiko mzuri wa kitimu.

Hata hivyo, timu hiyo inajivunia safu ya ulinzi inayoundwa na kipa Aishi Manula, Kelvin Yondani, Gadiel Michael, Mwaita Gereza na Bakari Mwamnyeto ambayo imekuwa imara.

Rekodi inaonyesha Kilimanjaro Stars imekuwa ikipata wakati mgumu dhidi ya Uganda katika mashindano ya Chalenji. Katika mechi tano za mwisho Uganda imeshinda mara tatu na Kilimanjaro Stars mbili.

Mwaka 2013 Kilimanjaro Stars ilishinda kwa penalti 3-2 baada ya kutoka sare ya mabao 2-2. Katika nusu fainali mwaka 2010, ilishinda penalti 5-4 baada ya kutoka kutoka suluhu muda wa kawaida.

Mara zote tatu ambazo Uganda imepata ushindi, matokeo hayo yalikuwa katika muda wa kawaida wa mchezo ikishinda mabao 3-0 katika nusu fainali ya mwaka 2012. Nusu fainali ya mwaka 2011 ilishinda 3-1. Pia katika mashindano ya mwaka 2009 zilivaana katika makundi ambapo Uganda ilishinda mabao 2-0.

Akizungumza jana, Kocha wa Uganda, Jonathan McKinstry alisema hawaidharau Kilimanjaro Stars katika mchezo huo.

“Siku zote mechi baina ya Uganda na Tanzania ni ngumu na mara ya mwisho timu hizi kukutana Uganda tulipoteza, hivyo hata mchezo huu wa nusu fainali sidhani kama utakuwa rahisi ukizingatia pia wachezaji wangu wamecheza mechi nne mfululizo bila kupata nafasi ya kutosha kujiweka sawa na umri wao wengi ni wadogo.

“Hata hivyo tumejiandaa vizuri kuona ni kwa namna gani tutaibuka na ushindi dhidi yao na tuweze kutinga hatua ya fainali,” alisema McKinstry

Kocha wa Kilimanjaro Stars, Juma Mgunda alisema kuwa timu yake haina presha wala hofu ya kukabiliana na wenyeji katika mchezo wa leo.

Chanzo: mwananchi.co.tz