Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kili Queens, Kenya fainali ya wababe

85639 Pic+kili Kili Queens, Kenya fainali ya wababe

Sun, 24 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Unaweza kusema ni fainali ya wababe katika michuano ya Cecafa kwa upande wa wanawake inayohitimishwa kesho, ambapo timu ya taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Queens itaikabili ile ya Kenya, Harambee Starlets katika mchezo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini hapa.

Katika mechi za nusu fainali zilizochezwa jana, Kilimanjaro Queens iliifunga Uganda bao 1-0 lililotupiwa kimiani na mshambuliaji Asha Rashid ‘Mwalala’ katika dakika ya 90 huku Starlets ikiiadhibu Burundi kwa mabao 5-0.

Fainali ya kesho inazikutanisha timu hizo ambazo pia ziliongoza katika makundi yao kuwania kutinga nusu fainali, ambapo Kilimanjaro Queens iliyokuwa kundi ‘A’ ilizifunga Sudan Kusini mabao 9-0, Zanzibar 7-0 na Burundi 4-0, huku Kenya ikizifumua Djibouti 12-0, Uganda 3-0 na Ethiopia 2-0.

Kwa ushindi huo fainali hiyo inatarajiwa kuwa ya kusisimua kutokana na timu hizo kila moja kufanya vizuri katika hatua ya makundi, licha ya kwamba Tanzania hadi jana ilikuwa imezifumania nyavu mara 21 ilhali Kenya ikiwa na jumla ya mabao 22.

Hata hivyo, Tanzania inajivunia kuwa mabingwa wanaoongoza kulitwaa kombe la michuano hiyo wakiwa wamelinyakua mara mbili mwaka 2016 na 2018, huku Zanzibar wakilitwaa mara moja mwaka 1986 kabla ya kusimamishwa kwa michuano hiyo kwa takriban miaka 30.

USHINDI WAO

Katika mechi ya jana, Kilimanjaro Queens ililazimika kusubiri hadi dakika ya 90 kupata bao lake lililofungwa na Asha kwa shuti kali baada ya kupokea pasi kutoka kwa Mwanahamisi Omary ‘Gaucho’ aliyekokota mpira kutokea upande wao wa kushoto.

Uganda ambayo ilionyesha upinzani mkali kwa Queens ilicheza mchezo safi huku ikilishambulia lango la wenyeji, lakini uimara wa safu ya ulinzi ya Tanzania Bara uliwanyima mabao.

Kwa upande wake, washambuliaji wa Bara walifanya mashambulizi mengi langoni mwa Uganda, lakini ama yaliishia kuokolewa au walikosa mabao.

Akizungumzia ushindi huo, kocha wa Tanzania Bara, Bakari Shime alisema: “Nimefurahi kutokana na kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wangu, lakini pia wapinzani wangu walijua mbinu nilizoingia nazo wakatuzuia (kupata mabao).” Pia aliwalalamikia wachezaji wa Uganda akidai walitumia mbinu ya kujidondosha mara kwa mara iliyopunguza kasi ya mchezo. “Walitumia mbinu hiyo ili kupoozesha mchezo, lakini mwisho wa siku tumemaliza na matokeo.”

Hata hivyo, kocha wa Uganda, Faridah Belega aligoma kuzungumzia mchezo huo akisema, “no comments (sina cha kuzungumza).”

Katika mchezo wa awali, Harambee Starlets wanaotamba na staa wao Mwanalima Jereko, walicheza kwa kiwango cha juu na kuwafanya Warundi wakubali matokeo kwa kipigo cha mabao 5-0.

Kenya ilipata mabao yake kupitia kwa Dorcas Nixon katika dakika ya tano, Jentrix Shikangwa dakika ya 54 na 71, Mwanalima dakika ya 67 na Carazone Aquino ya 77.

Burundi na Uganda watacheza mchezo wa kuwania mshindi wa tatu kesho kabla ya mchezo wa fainali.

Chanzo: mwananchi.co.tz