Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kila mtu apanga ratiba yake La Liga

68539 Liga+pic

Sun, 28 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Madrid, Hispania. Wiki za mwanzo za msimu wa soka nchini Hispania zimeingia matatizoni baada ya shirikisho la soka la nchi na Ligi Kuu (La Liga) kutangaza ratiba tofauti kutokana na uamuzi kuhusu mechi za mwishoni mwa wiki.

La Liga inataka kuendelea na mechi zinazopangwa kufanyika Ijumaa na Jumatatu msimu huu kwa ajili ya kampuni zinazotangaza ligi hiyo.

Baada ya Shirikisho la Soka la Hispania (RFEF) kujibu kuwa ndilo linalosimamia kalenda ya soka, kamati yake ilikubaliana na msimamo huo, ikisubiri uamuzi wa mahakama ya kawaida.

La Liga ilishapanga ratiba ya mechi za wikiendi tatu za kwanza.

Lakini RFEF ilitangaza ratiba ya mechi inayorekebisha na La Liga ikatoa taarifa inayosema kuwa mechi hizo hazitahamishwa.

Barcelona na Athletic Bilbao zilipangwa kuanza mechi hizo Ijumaa ya Agosti 16, lakini RFEF ikasema sasa zitachezwa Jumamosi.

Pia ilibadilisha mechi mbili zilizopangwa kufanyika Jumatatu ya Agosti 19, ikisema Mallorca na Eibar zitacheza Jumamosi na Betis na Valladolid Jumapili.

Lakini La Liga ikasema yenyewe ndio chombo pekee chenye haki ya kupanga tarehe na siku za mechi za mashindano ya taifa ya ligi ya wachezaji wa kulipwa.

"Kwa hiyo, ratiba iliyokwishatolewa na La Liga kwa siku za kwanza za ligi ndizo mechi zitakazochezwa," inasema taarifa ya La Liga.

La Liga ilisema uamuzi huo wa RFEF unahatarisha mikataba ya kitaifa na kimataifa ya haki za televisheni yenye thamani ya "zaidi ya dola milioni 2.2 za Kimarekani".

Lakini RFEF ilisema inawakilisha utashi wa mashabiki wanaopinga mechi kuchezwa Jumatatu. Vyombo vya habari vya Hispania viliripoti kuwa RFEF ikom tayari kujadiliana kuhusu mechi za Ijumaa na inataka fedha zaidi kutoka La Liga.

Chanzo: mwananchi.co.tz