Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kila mchezaji wa kigeni mil 4

76d4507e3182e6986a6403a9b7ecb1cd Kila mchezaji wa kigeni mil 4

Tue, 11 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KLABU ya Ligi Kuu Tanzania Bara italazimika kulipa ada ya Sh milioni 40 kama itasajili wachezaji 10 wa kigeni, kwa mujibu wa maboresho yaliyofanywa na Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB).

Mtendaji Mkuu wa TPLB, Almas Kasongo, alisema jana kuwa, wamekubaliana na timu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, ada ya mchezaji mmoja wa kigeni kuwa Sh milioni 4 badala ya Sh milioni 2 za awali.

Klabu itakayosajili wachezaji 10 itabidi kujiminya zaidi na kutoa kiasi cha Sh milioni 40 badala ya milioni 20 za awali ili kuwasajili wachezaji hao kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili waweze kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mbali na kuongeza kiasi hicho cha ada, Bodi ya Ligi pia imerekebisha ratiba ya mechi za ligi hiyo, ambapo sasa mechi nyingi zitakuwa zikichezwa mwishoni mwa wiki ili kutoa nafasi zaidi ya timu kupata muda wa kusafiri na kujiandaa kwa mchezo unaofuata.

Kasongo alisema badala ya saa 72 kutoka mchezo mmoja na mwingine, sasa muda utaongezeka zaidi baada ya timu kupungua kutoka 20 hadi 18.

Aidha, alisema Ligi Kuu badala ya kuwa na mechi 380 kwa msimu, kuanzia msimu ujao mechi zitakuwa 306, hivyo itatoa nafasi kwa timu kuwa na muda zaidi wa kujiandaa kutoka mchezo mmoja hadi mwingine.

Alisema katikati ya wiki kutakuwa na mechi chache ili kuhakikisha timu zinapata nafasi ya kusafiri na kujiandaa kwa ajili ya mchezo ujao.

Kasongo pia alisema katika mabadiliko mapya, timu itatakiwa kuwasilisha orodha ya majina ya wachezaji wake watakaocheza na wa akiba kwa mchezo wa siku hiyo, awali timu ilitakiwa kuwasilisha majina hayo wakati wa mkutano kabla ya mechi (pre-match meeting), lakini sasa watawasilisha saa mbili kabla ya mchezo husika.

Alisema wameamua hivyo baada ya kubaini kanuni hiyo haikuwa rafiki, kwani timu nyingi zilikuwa zikipigwa faini baada ya kushindwa kuwasilisha majina hayo wakati wa mkutano huo wa kabla ya mchezo.

Chanzo: habarileo.co.tz