Arusha. Mwanariadha Alphonce Simbu, ametajwa ndiye mtu sahihi wa kushika nafasi ya Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT).
Katibu Mkuu wa RT, Wilhelm Gidabuday alisema Simbu ni mwanariadha mwenye shauku ya kuipa mafanikio Tanzania kupitia mchezo huo.
Akizungumza jana, Gidabuday alisema Simbu amekuwa mstari wa mbele kwa kutoa mchango wa kuhakikisha riadha inarejea katika kiwango bora kama zamani.
Gidabuday alisema ana amini Simbu atawania uongozi wa RT ndani ya miaka 10 ijayo kwa kuwa ni mwanariadha anayependa mabadiliko ya kiutendaji.
Alisema Simbu ana mkakati wa muda mrefu wa kuifikisha Tanzania katika medani ya kimataifa akitumia ushawishi baada ya kung’ara katika mashindano ya kimataifa.
“Miaka 10 au 20 baadaye namuona Simbu akiwa kwenye kiti changu akiendeleza gurudumu la maendeleo ya riadha na kiu yake kubwa ni kupata eneo la kujenga kituo cha mchezo huo,”alisema Gidabuday.
Hata hivyo, Simbu alisema anajiandaa na mashindano ya kimataifa na hakuwahi kufikiri kuwa kiongozi wa shirikisho hilo, baada ya kustaafu riadha.
“Kwa sasa nawaza namna ya kuvunja rekodi katika mbio za kimataifa na dunia kwa ujumla, masuala ya uongozi nawaachia watangulizi wangu sijawahi kufikiri jambo kama hilo,”alisema Simbu.
Aidha, mwanariadha huyo alisema Tanzania ina idadi kubwa ya wanariadha wenye vipaji, lakini wamekosa mkakati wa kuibua na kuendeleza vipaji, hivyo ametoa wito kwa wadau kuweka mkakati wa kusimamia vyema sekta ya michezo.