Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kichuya, Mauya kumchangia Mdamu

Mauya Pic Data Kichuya, Mauya kumchangia Mdamu

Fri, 30 Jul 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

MASTAA mbalimbali wa Ligi Kuu Bara akiwamo Shiza Kichuya na Zawadi Mauya wataungana na wale wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kucheza mchezo maalumu wa hisani ili kuchangia fedha za matibabu ya nyota mwenzao, Mathias Mdamu aliyevunjika miguu akiwa na timu ya Polisi Tanzania.

Mdamu alipatwa na mkasa huyo kwenye ajali iliyoikumba timu ya Polisi Julai 7 ikitoka mazoezini kujiandaa na mechi za mwisho za Ligi Kuu Bara, huku wenzake wakipata majeraha ya kawaida.

Katika kuhakikisha Mdamu anapata matibabu ya kumsaidia kulinda kipaji chake, imeandaliwa mechi maalumu ya kufanya harambee ya kuchangia matibabu ya mchezaji huyo wa zamani wa Mwadui.

Kwa mujibu wa mmoja wa waratibu wa mchezo huo, Nestory Tweve aliliambia Mwanaspoti kuwa wameandaa mchezo huo utakaopigwa wikiendi hii mjini Morogoro na kushirikisha timu za nyota wa Ligi Kuu na wale wa FDL, na baadhi yao ni Shiza Kichuya wa Namungo, Zawadi Mauya na Dickson Job wa Yanga.

“Wapo wachezaji wengi wameonyesha moyo na kuguswa na tukio la mwenzao ambaye anaonyesha kuwa na uhitaji mkubwa kwa ajili ya matibabu, kwa hiyo kama mdau kwa kushirikiana na wenzangu tuliona tuwaunganishe kwa mchezo huo,” alisema Tweve na kuongeza:

“Kila mwenye nia na dhumuni la dhati la kutaka kumsaidia Mdamu tunamuomba ajitokeze kuushuhudia mchezo huo na ukimalizika kilichopatikana tutaikabidhi familia yake kwa ajili ya kusaidia matibabu yake.”

Kuhusu utaratibu, Tweve alisema waliongea na uongozi wa Polisi Tanzania na kueleza dhamira yao kisha wakafanya mawasiliano na familia yake na hapakuwa na kipingamizi chochote, hivyo wakaona waunganishe nguvu pamoja na wachezaji ambao nao wamejitolea kwa upande wao.

“Chama cha Mkoa hakina shida, nadhani kati ya Ijumaa au Jumamosi watatupa uwanja (Sabasaba) kwa mchezo huo, maana tayari tumefanya nao mawasiliano na wamefurahishwa na mpango huo,” alisema mratibu wa mchezo huo wa hisani utakaochezwa Morogoro.

Mbali na Kichuya, Mauya na Job wengine ambao wanatajwa kuwa sehemu ya mchezo huo ni kipa wa Mbeya City, Haruna Mandanda, Kibwana Shomary wa Yanga, Salum Kihimbwa, Jafar Kibaya wa Mtibwa Sugar na wengine kibao.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz