Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kibaya apiga tatu, Mtibwa Sugar yapiga 4G

29157 Mtibwa+pic TanzaniaWeb

Wed, 28 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mabao matatu ya mshambuliaji Jaffary Kibaya yametosha kuipa Mtibwa Sugar ushindi mnono wa magoli 4-0 dhidi ya Northern Dynamo katika mchezo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi.

Katika mchezo huo mabao ya Mtibwa Sugar yalifungwa na Kibaya aliyefunga mabao matatu katika dakika ya 13, 35, 58 na Riphat Khamis alifunga bao la mwisho dakika 90.

Ushindi huo unaifanya Mtibwa Sugar kuwa katika mazingira mazuri ya kufuzu iwapo itapata sare au kufungwa chini ya mabao nne katika mchezo wa marudiano utakaofanyika Shelisheli.

Iwapo Mtibwa Sugar itasonga mbele kwa raundi inayofuata itacheza dhidi ya KCCA ya Uganda hapo Desemba 16.

Katika mchezo huo Mtibwa imeweka rekodi ya kupiga mashuti 38 golini na kufanikiwa kupata mabao manne.

Mtibwa Sugar ilitumia dakika 13 kulishambulia lango la wapinzani kabla ya kupata bao la kuongoza lililofungwa na Kibaya akitumia vizuri uzembe wa mabeki Dynamo.

Dakika 14, Northern Dynamo ilifika langoni kwa Mtibwa Sugar, lakini umakini wa kipa wa Mtibwa Sugar, Shabaan Kado ulisaidia kulinda lango.

Kibaya alifunga bao lake la pili baada ya kumpiga chenga beki wa Dynamo na kupiga shuti kali akiwa pembeni lililokwenda moja kwa moja wavuni katika dakika 35.

Mtibwa Sugar itajilaumu wenyewe kwa kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao mawili baada ya washambuliaji wake kukosa umakini wa kumalizia nafasi nyingi walizozipata katika kipindi cha kwanza.

Bao Kibaya limewasahaurisha hasira mashabiki ambao walikuwa wanamtolea maneno makali Juma Luizio kwa kukosa mabao mawili ya wazi dakika ya 33 na 34.

Hata hivyo dakika ya 38 Luizio alirekebisha makosa baada ya kumchongea pasi nzuri Ismal Aidan ambaye alikosa utulivu akapiga shuti la juu.

Kocha wa Mtibwa Sugar, Zuber Katwila na Mkurugenzi wa ufundi la Mtibwa Sugar, Salum Mayanga muda mwingi wa mchezo alikuwa akiwatuliza wachezaji wake walionekana kuwa na presha ya kila mmoja kutaka kufunga.

Northern Dynamo iliyoingia katika mchezo huo kwa mbinu ya kujilinda kwa kuchezesha viungo watano na mabeki wanne, mbinu iliyosaidia kwa kiasi hadi mapumziko.

Kipindi cha pili dakika 58, Kibaya alifunga bao lake la tatu kwa mkwaju wa penalti baada ya Khamis kuangushwa kwenye eneo la hatari na beki wa Dynamo.

Mtibwa iliendelea kupoteza na hadi dakika ya 90+1, Riphat aliporekebisha makosa yake kwa kufunga bao la nne baada ya kuwatoka mabeki na kupiga shuti lililomshinda kipa na kujaa wavuni.

Kocha wa Mtibwa Sugar, Katwila amesema ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Northern Dynamo umewaweka kwenye mazingira mazuri ya kusonga mbele.

Katwila amesema katika mechi ya marudiano kazi yao kubwa itakuwa kulinda ushindi walioupata.

"Tutajiandaa kikamilifu mechi ya ugenini, hatuwezi kuwadharau Northern Dynamo kwa kuwafunga mabao 4-0 hatuwezi kujua kwao watakuaje," alisema Katwila.

Mbali na kuzungumzia ushindi walioupata alikemea kitendo cha washambuliaji wake kuonyesha papara na kupoteza nafasi nyingi za wazi.

"Tulikuwa na nafasi ya kufunga mabao zaidi ya 4-0 sijui niseme papara, dharau ama kulewa sifa, lakini nitaenda kufanyia kazi mapungufu hayo.

"Tunahitaji kusonga mbele zaidi kwani tunaiwakilisha Tanzania hivyo tunaomba kuungwa mkono na mashabiki kama walivyofanya mechi ya leo," alisema Katwila.



Chanzo: mwananchi.co.tz