Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kiba apewa mikoba Coastal

16121 Pic+kiba TanzaniaWeb

Fri, 7 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’ Ali Kiba anatarajiwa kuongoza mashambulizi katika mchezo dhidi ya African Lyon, Septemba 14.

Kocha wa Coastal, Juma Mgunda alisema Kiba ataongoza mashambulizi katika mchezo huo ambao utakuwa wa kwanza kwake msimu huu katika mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akizungumza kwa simu jana, Mgunda alisema Kiba ambaye ni msanii nyota wa muziki wa bongo fleva, ameonyesha uwezo mzuri kwenye mazoezi ya kikosi hicho.

“Kiba ana uwezo mkubwa wa kucheza namba 9 au 10 nitamtumia kwa mara ya kwanza katika mchezo na Lyon, yuko vizuri hatukukosea kumsajili,”alisema kocha Mgunda.

Kocha huyo alisema mchezaji huyo alikosa mechi mbili dhidi ya Lipuli walitoka sare ya bao 1-1 kabla ya kuilaza Biashara United 1-0, katika mechi zote mbili zilizochezwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Coastal na Taifa Stars, alisema Kiba alikosa mechi hizo kutokana na sababu binafsi ambazo zilimuweka nje ya kituo cha kazi.

“Ni mchezaji mwenye kipaji namfahamu tangu akicheza timu za Kariakoo kabla hajahamia Kinondoni, japo muziki ndiyo ulimpa umaarufu, lakini ana kipaji kwenye mazoezi yetu ameonyesha uwezo mzuri,” alisema Mgunda.

Coastal itakuwa ugenini kwa mara ya kwanza katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu ambapo itakuwa jijini Dar es Salaam kupepetana na African Lyon.

Chanzo: mwananchi.co.tz