Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kerr kikwazo dili la Kagere kutua Yanga

9373 Pic+kerr TZW

Sat, 16 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Uwezekano wa Yanga kumnasa mfungaji bora wa mashindano ya SportPesa Super Cup, Meddie Kagere umeanza kuwa finyu baada ya klabu yake ya Gor Mahia kutangaza kuwa wanamuandalia mkataba mnono.

Mabingwa hao wa Ligi Kuu Kenya, wametangaza hilo huku Kagere akiwindwa na Yanga iliyovutiwa na kiwango chake.

“Kwa sasa nasema hivi hawezi kuondoka. Tunamhitaji atusaidie kutetea ubingwa wetu wa Ligi Kuu na pia pia awe msaada wa kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.. Mwisho wa msimu mkataba wake utakapomalizika hapo sasa ndio uongozi utaamua kama ataongeza mkataba au tutamuachia aondoke,” alisema Kocha wa Gor Mahia, Dylan Kerr.

Yanga wanatamani kumsajili nyota huyo ili kuimarisha safu yake ya ushambuliaji ambayo msimu uliopita haikuonyesha makali kiasi cha kushindwa kufanya vema katika Ligi kuu Tanzania bara na Kombe la Shirikisho.

Hesabu kubwa kwa Yanga ni kutaka asimame mbele na Obrey Chirwa kutengeneza safu moja matata lakini hali hiyo haipo tena.

Inaonekana kuwa Yanga imekuwa ikimfatilia Kagere kimyakimya ikilenga kumsajili ili azibe pengo lililoachwa na Donald Ngoma aliyetimkia Azam.

Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa alifichua kuwa mshambuliaji huyo wa Gor Mahia anahitaji fungu kubwa la fedha ili ajiunge na Yanga. “Ni kweli tuna tatizo katika nafasi ya kipa na ushambuliaji ambayo ni lazima tuzijaze kwa kupata wachezaji hodari ambao wataisaidia Yanga kulingana na mahitaji ya timu, lakini fedha anazotaka Kagere ni nyingi hatuwezi kutoa japo mazungumzo yanawezekana,” alisema Mkwasa.

Mbali ya klabu ya Gor Mahi kutangaza nia ya kumuongezea mkataba mshambuliaji huyo amethibitisha kuanza kwa mchakato wa kusaini mkataba mpya ili aendelee kuitumikia Gor Mahia.

Mshambuliaji huyo aliuambia mtandao wa Gor Mahia juzi kuwa yuko tayari kubakia kwenye klabu hiyo iwapo watafikia makubaliano baina yake na uongozi.

“Nilisaini mkataba wa muda mfupi na Gor Mahia lakini nipo tayari kusikiliza kitu gani wamejiandaa kunipatia ili nisaini mkataba mpya na kama tutafikia maelewano juu ya kile ninachokihitaji, bila shaka yoyote nitabakia na ninatoa mchango wangu wa hali ya juu kwa timu,” alisema Kagere.

Jina la Kagere lilianza kuteka hisia za vyombo vya habari nchini baada ya kuibuka mfungaji bora wa mashindano ya SportPesa Super Cup yaliyomalizika nchini Kenya wiki iliyopita kutokana na mabao yake manne aliyoifungia Gor Mahia katika mechi tatu ilizocheza dhidi ya timu za JKU, Singida United na Simba kuipa ubingwa.

Safu ya ushambuliaji ya Yanga kwa msimu uliopita iliwategemea zaidi Obrey Chirwa na Ibrahim Ajibu baada ya Ngoma na Amissi Tambwe kuwa nje ya dimba kwa kipindi kirefu. Tayari wawakilishi hao wa Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho wamemleta nchini mshambuliaji raia wa Benin, Marcelin Koupko kwa ajili ya kumsainisha mkataba wakilenga kuongeza nguvu ingawa kuna tetesi kuwa Chirwa ambaye mkataba wake umemalizika, anafanya mipango ya kwenda kukipiga nje ya nchi.

Nyota wengine ambao wamekuwa wakiwindwa na Yanga katika dirisha hili la usajili mbali ya Kagere ni viungo wa Simba, Mohammed Ibrahim na kiungo Said Ndemla pamoja na kipa wa Mtibwa, aliyepata kupitia klabuni hapo Benedictor Tinoco.

Chanzo: mwananchi.co.tz