Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kazi imeanza Yanga: Pacha wa Yondani huyu huyu hapa

15524 PIC+PACHA TanzaniaWeb

Tue, 4 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera tayari ametua Liberia ili kuiongoza timu yake ya taifa lake la DR Congo dhidi ya wenyeji wao, lakini wakati akiondoka nchini aliagiza atafutiwe haraka beki wa kati atakayechuana na Kelvin Yondani.

Mabosi wa Kamati ya Usajili wa Yanga wala hawakutaka kulaza damu, kwani wameanza kulifanyia kazi agizo hilo kwa kuanza na beki mtata aliyemficha straika wao, Heritier Makambo katika mechi yao ya mwisho ya michuano ya CAF.

Katika ripoti ya kocha Zahera aliagiza atafutiwe beki wa kulia, wa kati na mastraika wa maana ili kuhakikisha kikosi chake kinaenea ipasavyo kwa ushindani.

Sasa kwa kuanza bosi wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika aliianza kazi hiyo mjini Kigali kwa kutua kwa beki wa kati na nahodha wa Rayon Sports, Abdul Rwatubyaye ambaye katika mechi yao hakubali kirahisi kupitwa na straika yeyote.

Kama mmesahau ni kwamba, beki huyo wakati akiichezea APR ya Rwanda alikaribia kutua Jangwani mwaka 2016 lakini mabosi wa Yanga walimuona bado ni beki kijana na kuahirisha dili hilo ili apate kwanza uzoefu.

Sasa unaambiwa kwa kazi kubwa aliyoifanya kwenye Uwanja wa Nyamirambo na kuifanya Yanga ilale bao 1-0 huku ikiwa na Makambo na Ibrahim Ajibu, kina Nyika wakaona hawezi kumuacha kirahisi kwani anaonekana atamfaa Kocha Zahera.

Kazi aliyofanya beki huyo kumficha Makambo ikawafanya kina Nyika kuchelewa kutoka uwanjani wakimsubiri beki huyo na kamera za Mwanaspoti lililokuwa

Kigali kuwaripotia mchezo huo liliwanasa wakiwekana sawa.

Nyika pamoja na Mjumbe wake, Hamad Islam walinaswa wakibadilishana namba na simu na beki huyo aliyekata hewa na ambayo kama akitua Jangwani na kuungana na Yondani, mastraika wa timu pinzani huenda wakapata tabu sana.

MSIKIENI MWENYEWE

Bila kujua walichokuwa wakizungumza, baada ya muda watu hao watatu waliachana wakiwa na furaha za bashasha na Mwanaspoti halikumuacha bure beki huyo ila kumvamia na kuzungumza naye.

Rwatubyaye alikiri mabosi hao wameonyesha kuhitaji huduma yake, lakini kwa kuwa hawakuwa na muda mzuri wa kujadiliana kwa kina waliamua kupeana ahadi ya kuendelea na mazungumzo ndio maana walibadilishana namba za mawasiliano.

Beki huyo alisema kwa sasa bado ana mkataba na klabu yake ya Rayon, lakini hautamzuia kutua Yanga endapo mazungumzo yao yataendelea vizuri.

“Ni kweli wameonyesha nia ya kunihitaji wamesema nilicheza vizuri na sasa niko vizuri zaidi kuliko wakati ule walipofanya mazungumzo na mimi.

“Nimewaambia bado nina mkataba na Rayon, ila sidhani kama utanizuia kuondoka endapo tutakubaliana vizuri huko mbele. Ni hayo kwa sasa.”

Kocha Zahera anahitaji beki matata wa kusimama sambamba na Yondani ambaye pacha wake, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amestaafu na kuwa Meneja, huku Andrew

Vincent ‘Dante’ anayecheza naye akionekana bado hajavihimili vyema viatu.

BEKI MATATA

Beki huyo aliyezaliwa Oktoba 23, 1996 ikiwa na maana kwa sasa ana umri wa miaka 21 tu, mbali na kukipiga APR na sasa Rayon aliyojiunga nayo Julai mwaka jana, pia amewahi kukipiga Slovakia akiichezea klabu ya Topolcany.

Rwatubyaye ana urefu wa mita 1.82 na awapo uwanjani mbali na kutupia urefu wake kudhibiti mastraika wakorofi, lakini ni fundi wa kutumia nguvu, akili na ni mahiri zaidi kwa mipira ya juu, kitu ambacho mabosi wa Yanga wanadhani atakuwa msaada mkubwa katika kikosi chao kilichomaliza nafasi ya nne katika Kundi D la michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Chanzo: mwananchi.co.tz