Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kauli za wagombea ubunge CCM zaibua mjadala mzito

16439 Pic+kauli+ccm TanzaniaWeb

Sun, 9 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ikiwa imesalia wiki moja kabla ya kufanyika uchaguzi mdogo katika majimbo ya Ukonga na Monduli, miongoni mwa hoja za CCM ambazo zimechukua nafasi kubwa ya kampeni ni utetezi wa wagombea kuwa wamehamia katika chama hicho kufuata maendeleo.

Wagombea hao, Mwita Waitara wa Ukonga na Julius Kalanga wa Monduli, kwa nyakati tofauti wamekuwa wakitumia muda mwingi kuelezea sababu zao kuhama upinzani kwenda katika chama hicho tawala, kwamba ni kutafuta urahisi wa kuwahudumia wananchi wao na kuwaletea maendeleo.

Wagombea hao wawili walikuwa wabunge wa majimbo hayo kupitia Chadema, wakajiuzulu na kujiunga na CCM ambayo imewateua tena kuwania nafasi hizo.

Kauli ya Kalanga

Katika mikutano yake, Kalanga amekuwa akisema alijiuzulu ubunge kwa kuwa alikuwa na mkataba na wananchi kuwaletea maendeleo na sasa akiwa CCM atakuwa anawasiliana na serikali moja kwa moja.

Asemavyo Waitara

Waitara anasema baada ya kushindwa kutimiza majukumu ya msingi kama kiongozi wa upinzani kutokana na Chadema kumzuia kukutana na viongozi wa CCM, aliamua kujiunga na chama chenye mawaziri wenye dhamana ya fedha wanaohusika na umeme, maji, elimu na afya.

Akiwa kwenye mkutano eneo la Msongola na kwingineko, Waitara amekuwa akisema miongoni mwa shida alizokuwa anapata ni viongozi wa chama chake kutokubali kuwa John Magufuli ndiye Rais.

“Nilikuwa nakatazwa hata kuonana na Mkuu wa Wilaya Sophia Mjema, Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda na mawaziri wenye dhamana ya maji, umeme na afya. Nikifanya hivyo nitawekewa kikao, nitaonywa na kuitwa msaliti, nitawaletea vipi maendeleo bila kuonana na wenye fedha, ”amekuwa akihoji Waitara.

Dhana isiyo sahihi

Wakati wabunge hao wakisema hayo, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa George Shumbusho amepingana na dhana hiyo akisema kuwa upinzani wenye msimamo chanya ndio unachagiza maendeleo.

Bila kumtaja mtu yeyote, Shumbusho alisema iwapo viongozi wa upinzani wataondoka wote na kuhamia katika chama tawala, kila mmoja atagundua kuwa maendeleo hayawezi kuwapo bila changamoto.

“Kwa tafsiri ya maendeleo lazima kuwepo na changamoto, kama hakuna kitu cha kuiambia Serikali imekosea hapa, irekebishe pale bila shaka yenyewe italala.

“Na wakigundua hakuna wa kuwakosoa hawatafanya kitu, kwa nchi zetu upinzani chanya ni muhimu sana kuionyesha Serikali kuwa hapa siyo na hapa sawa,” alisema Profesa Shumbusho.

Alisema kwa namna yoyote ile upinzani ni muhimu, tofauti na hapo hakuna kitakachofanyika, walio madarakani watalala kwa sababu wanajua hakuna wa kuwahoji wala kuwaondoa.

“Tatizo lililopo ni njaa na kama mtu ameahidiwa na huko alipo hapati kitu lazima atafanya maamuzi .

“Lakini kwa mpinzani mwenye kazi nyingine kama Tundu Lissu ambaye ni wakili, hawezi kuingia kwenye mitego kama hiyo, lakini ambaye siasa ndiyo inamlipa hana jinsi, zaidi ya kuhama akapate mkate wa siku,” alisema Profesa Shumbusho.

Kauli ya Profesa Shumbusho inaungwa mkono na mgombea wa Jimbo la Ukonga kupitia tiketi CUF, Salama Masudi anayejinadi kuwa iwapo atapata ridhaa ya kuongoza wananchi wa Ukonga ataishinikiza Serikali kuleta maendeleo.

Alisema atashirikiana na Serikali akiwa kwenye chama chake na kuishinikiza ilete maendeleo kwa wana Ukonga kwa sababu fedha zinazotumika kufanya hivyo ni kodi ya wananchi wote na kila mmoja ana haki nazo.

“Sitahama huku nilipo, nitashirikiana na Serikali nikiwa huku kuikumbusha kuwa wananchi wanataka maendeleo ambayo ni haki yao kwa sababu wanatozwa kodi.

“Kwangu hiyo ndiyo njia sahihi, sitowaacha njiani kwa tamaa ya chochote kile, maendeleo ni haki yenu na inafahamika wazi,” alisema Masudi.

Masudi alifafanua kuwa hata ujenzi wa barabara, umeme, maji, vyote vinafanyika kwa fedha ya kodi ya wananchi na siyo chama, hivyo kama mbunge jukumu lake itakuwa ni kuwakumbusha kufanya hivyo kadri awezavyo.

Hoja hizo pia zinagusiwa na Waziri Mkuu mstaafu FredrickSumaye ambaye pia ni mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, kuwa ukiwa miongoni mwao lazima ukubaliane nao.

Akimnadi mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chadema, Asia Msangi katika Uwanja wa Gulukwalala Gongolamboto, Sumaye alisema kwa nchi hii hakuna mahali unaweza kuikosoa Serikali, ikiwa hauko katika upinzani.

Alisema wanaohama upinzani kwa madai ya kwenda kuleta maendeleo akiwamo Waitara ni waongo kwa sababu wakiwa CCM siyo rahisi kuibana Serikali.

Alifafanua kuwa duniani kote inafahamika wapinzani ndiyo wanaichagiza Serikali kuwaletea wananchi maendeleo, hivyo anayekwenda huko kwa madai hayo anawalaghai.

“Wananchi wa Ukonga kuweni makini na mtu huyu, anawalaghai, ameshindwa kuibana Serikali akiwa upinzani akienda huko ndiyo anazibwa mdomo kabisa,” alisema.

Kauli hizo zinapingwa na katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole aliyesema kuwa Ukonga sasa maendeleo yanakuja kama kukanyaga ganda la ndizi kwa sababu Waitara akipiga simu moja kwa waziri mkuu inapokelewa.

Akiwa kwenye mkutano wa kumnadi Waitara kwenye eneo la Msongola A, alisema mgombea huyo ana nafasi ya kuwaletea wananchi maendeleo kwa sababu wanazungumza lugha moja na Serikali.

Alisema kwa sasa anayo nafasi ya kupiga simu moja tu kwa Rais Magufuli na akazungumza naye, hivyo ni rahisi kumueleza anachotaka na kikafanyika.

Aliwataka wana Ukonga wampe kura Waitara kwa sababu yupo sehemu sahihi, tofauti na wakati ule alipokuwa upande wa wanaomtukana Rais.

“Huyu (Waitara) ni muungwana ameamua kuja huku na sisi tumemrudisha tena kwenu ili awaletee maendeleo,” alisema Polepole, kauli ambayo haina tofauti sana na zinazotolewa na wale wanaomnadi Kalanga Monduli.

Chanzo: mwananchi.co.tz