Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kauli ya Karia yaibua mjadala

9884 Pic+karia TanzaniaWeb

Fri, 3 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Siku chache baada ya Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia kutoa kauli ya utata kwa klabu ya Yanga, baadhi ya wadau wa michezo wamekosoa matamshi yake.

Juzi, Karia akizungumza na gazeti hili, alidai Yanga haina sababu ya kutafuta visingizio, baada ya kufungwa mabao 3-2 na Gor Mahia ya Kenya katika mchezo wa Kombe la Shirikisho la Soka Afrika.

Karia alidai kitendo cha wachezaji kuchukuliwa kwenda kupiga picha za matangazo hakiwezi kuwa sababu ya kipigo hicho na alihoji kufungwa 4-0 ugenini kama kulichangiwa na shirikisho hilo.

Saa chache kabla ya Yanga kuivaa Gor Mahia, wachezaji watano waandamizi, walichukuliwa na TFF kwenda kupiga picha za matangazo ya timu ya Taifa ambako walitumia saa 11 kabla ya kurejeshwa kambini.

Kauli ya Karia dhidi ya Yanga imenukuliwa kwa mtazamo tofauti na wadau wa soka nchini ambao walihoji kama kiongozi huyo wa taasisi nyeti ana dhamira ya kuleta maendeleo ya soka.

Baadhi ya wadau waliozungumza na gazeti hili, walisema rais huyo hakupaswa kutoa kauli ya kuibeza Yanga kwa kuwa klabu hiyo ilikuwa inawakilisha Taifa.

Wengine walidai Karia alitakiwa kuituliza Yanga kwa kuwa TFF ina wajibu wa kutetea klabu zote nchini bila kujali ‘itikadi’ za viongozi ndani ya taasisi hiyo.

Kauli ya rais huyo imemuibua aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa TFF, Frederick Mwakalebela ambaye alisema kauli ya Karia ina ukakasi katika mustakabali wa soka nchini.

“TFF kama baba wa mpira ilipaswa kuipa sapoti ya kutosha Yanga katika mechi zao za kimataifa, uwepo wa Ligi Kuu lengo lake ni kupata timu zitakazowakilisha nchi na shirikisho lione matunda yake.

“Ni kweli Yanga ilifungwa Kenya na hata kwenda kupiga picha inaweza isiwe sababu ya kufungwa, lakini TFF iliisapoti vipi timu hiyo katika mchezo huo? kwenye hilo hawezi kukwepa lawama na kauli kwamba walifungwa Kenya sio nzuri,” alisema Mwakalebela.

Katibu wa Baraza la Wazee Yanga, Ibrahim Akilimali alisema kauli hiyo haikupaswa kutolewa na rais wa TFF na shirikisho hilo halikutakiwa kuwachukua wachezaji kambini wakiwa wanajiandaa kucheza mechi kubwa ya kimataifa.

“Hata angekuwa baba wa nyumba kwa kauli ile kwa mtoto inaonyesha dhana ya upendeleo kwa namna moja au nyingine, japo sitaki kuamini hivyo, si kauli nzuri hata kidogo,” alisema Akilimali.

Mwenyekiti wa zamani wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Kanali Mstaafu Idd Kipingu alisema tukio la kuwachukua wachezaji kambini halikuwa sahihi ingawa alishauri kauli ya Karia dhidi ya Yanga ipite.

“TFF ingekubali kuwa haikufanya sahihi, lakini pia inafikirisha kama kusingekuwa na hilo Yanga ingeshinda?, mapungufu ya Yanga yanajulikana japo tukio la wachezaji kuchukuliwa kambini linaweza kuwa moja ya kasoro ambazo tusingependa zijitokeze hata kwa timu nyingine.

Aliyewahi kuwa Rais wa Simba, Ismail Aden Rage alisita kutoa maoni akidai kauli yake dhidi ya kigogo huyo wa TFF inaweza kuchukuliwa kama mahakama ya rufani.

Karia alitoa kauli hiyo baada ya kocha msaidizi wa Yanga, Noel Mwandila kudai TFF ilichangia kipigo hicho kwa kuwachukua baadhi ya wachezaji kambini kwenda kupiga picha na kuwarudisha saa sita usiku kabla ya mchezo.

TFF iliwachukua kambini Deus Kaseke, Raphael Daud, Andrew Vincent ‘Dante’, Gadiel Michael na Ibrahim Ajibu kwenda kupiga picha za matangazo ya udhamini wa Taifa Stars kuanzia saa nane mchana na kuwarudisha saa sita usiku.

Kitendo hicho kilitajwa na Mwandila kilichangia kuivuruga timu hiyo kwa kuwa wachezaji walicheza wakiwa na uchovu. Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Kenya, Yanga ilicharazwa mabao 4-0.

Chanzo: mwananchi.co.tz