Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kauli 10 za Magufuli michezoni

Magufulii 660x370 Kauli 10 za Magufuli michezoni

Sat, 20 Mar 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

TANZANIA ipo katika maombolezo ya siku 14 ya kifo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli (JPM) aliyefariki majuzi Dar es Salaam kwa maradhi ya moyo.

Ni pigo kubwa kwa Taifa na sekta ya michezo ni miongoni mwa zilizoguswa na kifo hicho kutokana na mchango na mapenzi makubwa enzi za uhai wake katika tasnia hiyo sambamba na ndoto zake za kutaka kuona inapiga hatua.

Mwanaspoti inakuletea kauli 10 tofauti ambazo Rais Magufuli aliwahi kuzitoa kuhusu zinazogusa sekta ya michezo kwa nyakati tofauti.

AIJAZA UPEPO SIMBA

Mei 19, 2018, Rais Magufuli aliishuhudia Simba ikitobolewa tundu moja na Kagera Sugar katika mechi ya kukabidhiwa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na katika hotuba yake kabla ya kuwakabidhia kombe lao, JMP aliwachana kauli ambayo kwa kiasi fulani iliwajaza upepo Wekundu wa Msimbazi.

JPM aliichana Simba kwa soka bovu walililocheza mbele ya Kagera na kufungwa bao 1-0, lakini akawaambia ni lazima wakabadilike kama kweli wanataka kubeba ubingwa wa Afrika.

“Niwaombe Simba mkawe wa kwanza kuniletea ubingwa wa Afrika. Kwa mpira wa leo niliouona hamuwezi kuchukua ubingwa wa Afrika, lazima mbadilike,” alisema Rais Magufuli, kauli ambayo iliwatia nguvu Simba na kukomaa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika 2018-2019 kwa kufika robo fainali na msimu huu pia ikiwa imeshatanguliza mguu mmoja katika hatua hiyo.

UWANJA WA TAIFA

Wakati wa shughuli ya kuaga kitaifa mwili wa Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Mkapa kwa viongozi na wananchi iliyofanyika katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Julai 28,2020, Rais Magufuli aliagiza uilokuwa ukiitwa Uwanja wa Taifa kubadilishwa jina na kuwa Benjami Mkapa kama sehemu ya kumuenzi marehemu Mkapa, aliyetoa wazo na seriokali yake kuchangia ujenzi wa uwanja huo.

“Wengi wanataka Uwanja ule uitwe Uwanja wa Mkapa, ninajua hakupenda sana vitu viitwe kwa jina lake, lakini sasa hawezi niadhibu natamka rasmi utaitwa Uwanja wa Mkapa ili tuweze kumuenzi na kumkumbuka kwa kazi kubwa aliyoifanya kwa ajili ya kuendeleza maslahi ya michezo kwa taifa letu,” alisema Rais Magufuli.

MKWARA KWA STARS

Oktoba 19, 2018, Rais Magufuli mara baada ya kuipa fedha kiasi cha Shilingi 50 milioni, Taifa Stars, aliitaka kuhakikisha inapata ushindi katika mchezo wake wa ugenini wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika dhidi ya Lesotho.

“Fedha (Sh 50 milioni), nilizotoa zitumike kwa wachezaji, nataka ushindi, mkishindwa mtazitapika kwa njia nyingine,” alisema Rais Magufuli na kweli Stars iklafanya kweli na kufuzu fainali za Afcon 2019 iliyofanyika Cairo, Misri.

UWANJA MKUU WA DODOMA

Katika kudhihirisha kiu yake ya kutaka kuona michezo inapiga hatua, Oktoba 24, 2016, Rais Magufuli aliahidi kujengwa kwa Uwanja mkubwa na wa kisasa wa michezo jijini Dodoma, mradi ambao ungekuwa chini ya ufadhili wa serikali ya Morocco.

“Mbali na mikataba baina ya Tanzania na Morocco nimezungumza mambo mbalimbali na Mfalme Mohamed VI wa Morocco na nimemuomba atujengee Uwanja mkubwa wa mpira pale Makao Makuu yetu Dodoma utakaokuwa na thamani kati ya dola milioni 80 hadi 100 na amesema ataujenga, kwa hiyo utakuwa Uwanja mkubwa kuliko wa Dar es Salaam,” alisema Rais Magufuli.

BILIONI 1 ZA SERENGETI

Katika kufanikisha maandalizi ya timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’ kwa ajili ya ushiriki wa fainali za Afrika kwa vijana wa umri huo zilizofanyika nchini, mwaka 2019, Machi 25, 2019, Rais Magufuli alitoa kiasi cha Sh 1 bilioni kwenda Wizara inayohusika na michezo.

“Nikimwaga hela (fedha) hapa na nyinyi lazima mkamwage magoli ili kufikia malengo mliyoniahidi,” alisema Rais Magufuli.

BAJETI TIMU ZA TAIFA

Wakati wa hotuba ya ufunguzi wa Bunge la 12 jijini Dodoma, Novemba 13, 2020, Rais Magufuli aliahidi serikali kuanza kutoa fedha kwa ajili ya kusaidia maandalizi ya timu za taifa

“Tutaanza kutenga fedha kidogo kidogo kwa ajili ya kuzianda timu zetu za Taifa na katika hilo napenda kutumia fursa hii, kuitakia heri timu yetu ya Taifa kwenye mechi yao dhidi ya Tunisia hapo baadaye,” alisema Magufuli.

ANGALIZO KWA KINA BASHUNGWA

Desemba 9, 2020, Rais Magufuli alimpa angalizo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashingwa na msaidizi wake, Abdallah Ulega wakati akiwaapisha juu ya kuhakikisha suala la Usimba na Uyanga linaondoka kwenye timu ya Taifa na kuhakikisha wanaleta maendeleo ya soka

“Bashungwa tumekupeleka kwenye michezo tunataka tushinde, sio tukilala tukiamka mabao kumi, wote mtaondoka wewe na Naibu Waziri wako, wakati sasa umefika tuondokane na Usimba na Yanga umetuchelewesha sana, sisi tunataka kushinda na michezo iweze na matokeo na itoe ajira,” alisema Rais Magufuli.

AFAGILIA SAMATTA

Muda mfupi baada ya Mbwana Samatta kujiunga na KRC Genk ya Ubelgiji akitokea TP Mazembe ya DR Congo mwaka 2016, Rais Magufuli alimpongeza mshambuliaji huyo wa Kitanzania ambaye kwa sasa anachezea Fenerbahce ya Uturuki.

“Nimefurahishwa na mafanikio anayoendelea kuyapata Mbwana Samatta, nawaomba wanasoka wote Tanzania wayachukue mafanikio haya kama changamoto ya kufanya vizuri na kuzivutia timu mbalimbali za ndani na nje ya nchi,” alisema Rais Magufuli

AGAWA VIWANJA

Mara baada ya Taifa Stars kujihakikishia kufuzu Fainali za Afcon 2019, Rais Magufuli aliandaa chakula cha mchana Ikulu jijini Dar es Salaam na kuahidi kuwapa viwanja wachezaji wa kikosi hicho

“Kama tumeweza kuwapatia mabalozi viwanja, hatuwezi kushindwa kuwapatia mabalozi mnaoiwakilisha nchi hii katika machuano mbalimbali viwanja vya kujenga. Wanapostaafu, miguu inapokataa kupiga mipira, maisha yao yasiwe ya ajabu. Kwa kushirikiana na Katibu Mkuu mchukue majina yao pamoja na Mbwana Samatta ambaye ameondoka jana usiku, msimsahau na hicho kiwanja ukiamua kukiuza ni shauri yako lakini nataka sisi kama Serikali kwa niaba ya Watanzania iwe kama shukrani yetu kwenu,” alisema Rais Magufuli.

ZAWADI KWA TINO

Machi 25, 2018, Rais Magufuli alimpa zawadi ya fedha kiasi cha Sh 5 milioni mchezaji wa zamani wa Taifa Stars, Augustino Peter ‘Tino’ kama pongezi kwa kufunga bao lililoiongoza timu hiyo kufuzu Afcon kwa mara ya kwanza mwaka 1980.

“Kwa nafasi ya kipekee labda nimuombe Tino aje hapa mbele aseme kitu kwa ajili ya wenzake, na anaweza akatueleza changamoto maana tulikuwa tukisikia tu Peter Tino, Peter Tino. Kuna katibu hapa! Ebu mtafutie shilingi milioni tano huyu mzee ili akakuze mtaji wake,” alisema Rais Magufuli.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz