Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Katwila afuta ubingwa kwa Simba

12800 Pic+katwila TanzaniaWeb

Mon, 20 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati kocha wa Simba, Patrick Aussems akisema Simba hii haipoi baada ya kuifunga Mtibwa Sugar mabao 2-1 na kutwaa Ngao ya Jamii juzi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, kocha wa Mtibwa Sugar, Zubeir Katwila ameiangalia Simba na kusema ni ya kawaida sana na inaweza isitetee ubingwa wake.

Simba ilitetea ngao yake ya jamii jijini Mwanza ikiwa ni mchezo wa kukata utepe wa Ligi Kuu Bara.

Asemavyo kocha Mtibwa Sugar

Akizungumza jana kutoka Mwanza, Katwila alisema ushindi wa Simba ulichangiwa na uwingi wa mashabiki wao majukwaani lakini si mpira wa uwanjani.

Alisema Simba haikuwa tishio kwao licha ya kuwa na wachezaji kadhaa wa kigeni, lakini hawakucheza soka la kuwazidi,ingawa walishinda.

Katwila mwenye jeuri ya Kombe la FA, alisema mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, hawakuwazidi kisoka kabisa...tumefungwa baada ya mabeki kujichanganya, lakini sijaona Simba ilichotuzidi ndani ya uwanja, lakini kimpira tulicheza sawa.”

Kiungo huyo wa zamani wa Mtibwa, alisisitiza kuwa Simba ina kasoro nyingi ambazo anaamini zisipofanyiwa kazi ndani ya siku mbili hizi isitarajie kutetea ubingwa wake Ligi Kuu kirahisi.

“Nimeiona Simba ni timu isiyotisha uwanjani licha ya kusifiwa sana, walioshuhudia mechi yetu ya jana ‘juzi’ bila shaka wameiona, bado inacheza katika kiwango cha kawaida licha ya kuwa na mastaa wa kigeni wengi na kupiga kambi nchini Uturuki na sisi tulikuwa Manungu tu hapo,” alisema.

Akizungumzia kilichoigharimu timu yake hadi kukosa ushindi, Katwila alisema ni kushindwa kuzitumia nafasi nzuri walizozitengeneza na kujichanganya kwa mabeki.

“Tunakwenda kwenye Ligi Kuu, huko ndiko kwenye ‘vita’ ya pointi, tunapaswa kujipanga na mchezo wa jana ‘juzi’ umenionyesha upungufu kadhaa ambao nitaurekebisha haraka iwezekanavyo,” alisema.

Kocha wa Simba

Wakati Katwila akisema hayo, kocha wa Simba, Patrick Aussems alisema: “Simba hii haipoi hata.”

Kocha huyo raia wa Ubelgiji alisema baada ya mchezo: “Kwanza ni mwanzo mzuri kwetu kutimiza lengo ambalo tulitaka kuchukua ubingwa huu ili kuongeza morali ya timu kuelekea katika maandalizi ya Ligi, mashindano ya kimataifa na michuano mingine yote ambayo Simba tutakuwepo msimu huu.

“Niwapongeze wachezaji kwa kazi kubwa walioifanya kwa kucheza chini ya maelekezo ambayo tulikuwa tukielekezana tangu tulipokuwa kambini Uturuki na hata yale makosa ambayo waliyafanya katika mechi tatu za kirafiki yalitosha kabisa kutupa mwanga wa kupata ushindi katika mechi hii.

“Wachezaji wote ambao nimewapa nafasi wametumika kama nilivyokuwa nataka na nguvu yetu sasa inaelekea katika Ligi ambapo tutacheza mechi ya kwanza na Tanzania Prison huku tukiwa na deni kubwa la ubingwa mtetezi wa ligi.”

Ngao ya Jamii

Kabla ya hapo Simba ilitwaa Ngao ya Jamii Agosti mwaka jana ikiwa ni ufunguzi wa Ligi Kuu msimu wa 2017/2019, ikatwaa ubingwa wa ligi msimu uliomalizika kabla ya kutetea tena ngao kwa ushindi wa juzi.

Matokeo ya mchezo wa juzi dhidi ya Mtibwa, yameanza kutoa matumaini kwa mashabiki, wapenzi na wanachama wa Simba wakiamini kuwa yanatoa chachu ya mafanikio kwenye msimu ujao ambao watashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la FA pamoja na Kombe la Mapinduzi.

Uimara wa Simba

Nguvu ya Simba inaanzia kwa upana wa kikosi chake ambacho kimesheheni nyota wa kiwango cha juu wanaoweza kubadili mchezo na kuamua matokeo ya mechi katika muda wowote ule ambapo kila nafasi ina zaidi ya wachezaji wawili wenye uwezo.

Pia Simba inabebwa zaidi na safu yake ya kiungo ambayo imekuwa ndio nguzo kuu ya kuvuruga mipango ya timu pinzani na kutengeneza nafasi za mabao pia katika kumuliki na kutawala mchezo.

Simba wameonyesha kuwa wana safu kali ya ushambuliaji ambayo imekuwa na uwezo wa kufunga mabao wakitumia nafasi na udhaifu wa mabeki wa upinzani.

Udhaifu

Simba, bado ina tatizo kwenye safu yao ya ulinzi na wakati mwingine kusababisha waruhusu nyavu zao kutikisika.

Bado hakuna muunganiko bora kwenye safu ya ulinzi ya Simba hasa kwa mabeki Erasto Nyoni na Paschal Wawa lakini pia kipa Aishi Manula amekuwa akijisahau na kuruhusu mabao yanayotafsiriwa na kuonekana kuwa ni mepesi.

Mtazamo

Kocha John Tegete alisema Simba inabebwa zaidi na uwepo wa kundi kubwa la wachezaji wenye uzoefu ingawa kiwango chake ndani ya uwanja bado hakionyeshi utofauti mkubwa na timu nyingine za Tanzania.

“Kama ulitazama vizuri mchezo ule, nadhani utakubaliana na mimi kwamba timu zote zilicheza vizuri na sio Simba wala Mtibwa ambayo ilionyesha kiwango cha juu zaidi kuliko nyingine.

“Kilichowasaidia Simba ambacho naamini kitakuwa silaha kwao ni uzoefu ambao wachezaji wake wanao hasa wa kutumia vizuri nafasi wanazopata kutokana na makosa ya timu pinzani,” alisema Tegete.

Chanzo: mwananchi.co.tz