Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Katibu TFF aishauri Yanga

50442 Yanga+pic

Thu, 4 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Katibu mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka (TFF), Angetile Osiah amelishauri Baraza la Wadhamini la Yanga kutopuuza taratibu za kikatiba wakati huu wanapojaribu kumaliza mgogoro wa Yanga uliosababisha uongozi mzima kujiuzulu.

Yanga iko katika mtego mkubwa wa kikatiba baada ya kamati nzima ya utendaji kujiuzulu na kutakiwa kuitisha uchaguzi mpya, huku kamati ya uchaguzi nayo ikukumbwa na tatizo hilo la wajumbe wote kujiuzulu, huku wanachama wawili wakiwa wamefungua kesi kupinga kadi za kielektroniki za uanachama na hivyo mahakama kuzuia uchaguzi.

Kwa mujibu wa Katiba ya Yanga, kamati ya utendaji ndiyo yenye mamlaka ya kutangaza tarehe ya uchaguzi na pia huteua kamati ya uchaguzi, jambo ambalo kwa sasa haliwezekani kutokana na uongozi kutokuwepo na hivyo kulilazimisha Baraza la Wadhamini kuteua viongozi wa muda pamoja na kamati ya uchaguzi.

Hayo yamemfanya katibu huyo wa zamani TFF, Osiah kulitahadharisha Baraza la Wadhamini.

“Nadhani kumekuwa na tatizo kubwa. Kila kunapotokea mgogoro huwa kuna jitihada za kuumaliza haraka bila ya kuzingatia vitu vidogovidogo ambavyo mara nyingi huwa vinaleta migogoro,” alisema Osiah katika mahojiano na MCL Digital.

Alisema pamoja na Yanga kukabiliwa na migogoro mara kwa mara, huu wa sasa ni mpya kwa kuwa uongozi mzima na wajumbe wa kamati ya uchaguzi wamejiuzulu, huku kukiwa na kesi mahakamani.

Alisema katika hali kama hiyo, kuitishwa kwa mkutano mkuu ni jambo muhimu kuliko kukimbilia kwenye uchaguzi.

“Nadhani walichotakiwa kufanya akina (Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini), George Mkuchika ni kuteua kamati ya uongozi, halafu unawaambia waitishe mkutano mkuu wa Yanga,” alisema Osiah.

Alisema kwa kuwa mkutano mkuu ndio chombo cha juu kinachoweza kufanya uamuzi mkubwa, kamati ya uongozi iende na hoja ya kuomba ridhaa ya wanachama kuendesha klabu kwa siku 90 au miezi miwili.

Alisema kwa kawaida kujaribu kutatua migogoro kwa kukimbilia kwenye uchaguzi, hukumbana na vikwazo vingi vinavyoweza kukwamisha uchaguzi muda mfupi kabla ya siku iliyokusudiwa.

“Nasema hivyo kwa sababu uzoefu unaonyesha kuwa unaweza uchaguzi ukafanyika leo, halafu baada ya miezi mwiili akaibuka mtu akasema mkutano haukuwa halali, au uongozi haukuwa halali kwa kuwa haukutokana na chombo halali kwa mujibu wa Katiba ya Yanga,” alisema Osiah.

Alisema ingawa itakuwa vigumu kukubali mamlaka ya atakayeitisha kwa kuangalia mazingira ya sasa, lakini kwa kuwa Baraza la Wadhamini ndio chombo pekee halali Yanga kwa sasa, linaweza kutumia fursa hiyo kuteua kamati itakayoitisha mkutano mkuu.

Osiah pia alizungumzia suala la kesi iliyofunguliwa na wanachama wawili, Juma Magoma na Athumani Nyumba ambao wanapinga kufanyika uchaguzi huo kwa madai unakwenda kinyume na katiba ya klabu hiyo ya mwaka 2010 ibara ya 7 inayozungumzia utaratibu wa uanachama ndani ya klabu hiyo.

“Kuna vitu vingi ambavyo havijakaa sawa na nimesikia TFF ikisema ile kesi haihusiani na shughuli yao. Inaweza ikawa haihusiani lakini pale kwenye chumba cha mkutano itahusika katika suala la wanachama na inaweza kutokea mzozo wa nani aingie na nani asiingie,” alisema.

Alisema chombo ambacho kinaweza kufanya uamuzi mkubwa kabisa wa mwisho kuhusu utaratibu mpya wa kutoa kadi ni mkutano mkuu na ukishafanya uamuzi suala la kadi ziwe za aina gani si tatizo.

Yanga iliingia makubaliano na Benki ya Posta na baadaye CRDB kwa ajili ya kuchukulia malipo ya wanachama wapya na kutoa kadi za kielektroniki, lakini wanachama hao wanadai kuwa utaratibu huo haufuati mwongozo wa katiba ya Yanga kwa kuwa wanachama wapya hawajadiliwi na vyombo vilivyopewa jukumu hilo.

Osiah pia alizungumzia suala la kamati ya uchaguzi ya TFF kusimamia uchaguzi, akisema hilo pia litakuwa tatizo jingine.

Alisema kazi ya kamati ya uchaguzi ya TFF ni kuisimamia na kuielekeza kamati ya uchaguzi ya mwanachama wake na si kuchukua mamlaka ya kuendesha uchaguzi.

“TFF inapaswa kuwa wasimamizi wa kamati ya Yanga na sio kuingiza mikono yake.” alisema Osiah.



Chanzo: mwananchi.co.tz