Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Katibu Mkuu Chaneta, Mkisi ajiuzulu

Mkisii Katibu Mkuu wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta), Rose Mkisi amejiuzulu

Tue, 5 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Katibu Mkuu wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta), Rose Mkisi amejiuzulu.

Mkisi amewasilisha barua ya kujiuzulu jana kwa kamati ya utendaji ya chombo hicho huku akitaja sababu ya kujiuzulu kuwa ni sintofahamu ya maandalizi ya timu ya taifa ya netiboli ya U-21 kwa ajili ya michuano ya Afrika nchini Afrika Kusini.

Uamuzi huo wa Mkisi umekuja mara baada ya kutuhumiwa kukiuka sheria na kanuni za uendeshaji wa vyama vya michezo nchini, ambapo alidaiwa kuikosoa serikali kupitia vyombo vya habari kwa kutounga mkono mchezo huo badala yake kuwekeza kwenye soka ambapo alikuwa kinyume na sheria na kanuni.

Hatua hiyo ilimfanya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro kuliagiza Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kumuita Mkisi kwenye kamati ya maadili ili kutoa ushahidi wa tuhuma zake.

Waziri Ndumbaro pia aliagiza kusitishwa kwa malipo yote na tiketi za ndege zilizoelekezwa kusaidia timu ya Taifa ya U-21 hadi hapo itakapotangazwa.

“Naiagiza BMT kumuita Mkisi kwenye Kamati ya Maadili, pia kuleta ushahidi wa tuhuma alizotoa dhidi ya Serikali wakati akihojiwa na chombo kimoja cha habari, isitishe malipo yote hasa ya tiketi za kwenda Afrika Kusini ambazo tayari zimeshalipwa. Aidha, katika kikao kijacho nitakachoitisha hivi karibuni ili kukutana na vyama na mashirikisho ya michezo wasishiriki hadi suala hili litakapopatiwa ufumbuzi,” alisema Ndumbaro.

Kuhusu kujiuzulu, Mkisi amesema kuwa hakuna sababu za kubishana na waziri kuhusu suala hilo, licha ya kutopewa nafasi ya kueleza kilichotokea.

“Kipande cha sauti kilichokuwa kikitambaa hakikupata muktadha kamili wa nilichokuwa nikisema, hivyo kusababisha upotoshaji wa taarifa. Mimi nikiwa kiongozi mtendaji wa Chaneta nimeamua kuwajibika kwa kujiuzulu nafasi yangu,” amesema Mkisi kwa njia ya simu.

Mwenyekiti wa Chaneta, Devotha Marwa amethibitisha kwamba anafahamu uamuzi huo, ingawa barua hiyo iliwasilishwa kwa katibu mkuu msaidizi wa bodi hiyo.

“Tutatoa taarifa rasmi kuhusu suala hilo kwani tayari tumeshamaliza kilichotokea,” amesema Marwa kwa njia ya simu.

Chanzo: Mwanaspoti