Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kaseke aiokoa Yanga Tanga

39957 Kaseke+pic Kaseke aiokoa Yanga Tanga

Tue, 5 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tanga. Mabadiliko yaliyofanywa na Mwinyi Zahera yameiokoa Yanga kupata kipigo dhidi ya Coastal Union, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Yanga ilipambana na kupata pointi moja, baada ya kulazimisha sare ya bao 1-1 katika mchezo mkali uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Mkwakani, Tanga.

Mbinu ya kocha Zahera ya kumtoa nahodha Ibrahim Ajibu dakika ya 70 ilizaa matunda, baada ya Deus Kaseke aliyetokea benchi kufunga bao la kusawazisha.

Muda mfupi baada ya Kaseke kuingia aliichangamsha Yanga na kufunga bao hilo dakika ya 76 kwa shuti akimalizia pasi ya Matheo Anthony.

Bao hilo hilo lilitanguliwa na lile la Coastal lililofungwa kwa mpira wa kichwa dakika ya 29 na Haji Ugando, kutokana na makosa ya mabeki.

Ugando alifunga bao hilo akimalizia krosi iliyopigwa na Ayoub Lyanga ambaye aliambaa na mpira huku akibanwa na mabeki watatu wa Yanga, lakini alipiga krosi iliyomkuta Ugando aliyemzidi maarifa beki Paul Godfrey.

Bao hilo ni muendelezo wa udhaifu wa mabeki wa Yanga Kelvin Yondani na Abdallah Shaibu ‘Ninja’ ambao mara kwa mara walijichanganya kuokoa hatari langoni mwao.

Siku chache kabla ya mchezo huo, Zahera alisema atafanyia kazi kasoro za mabeki wake wa kati ambao wamekuwa wakifanya makosa mara kwa mara.

Licha ya timu zote kucheza vizuri huku Yanga ikimiliki mpira kwa kiasi kikubwa, safu yake ya ushambuliaji iliyoongozwa na Heritier Makambo haikuwa makini langoni mwa Coastal.

Ubabe

Baada ya Yanga kuruhusu bao hilo mechi ilianza kutawaliwa na ubabe wa hapa na pale huku wachezaji wakichezeana madhambi.

Dakika ya 74 Issa Abushehe wa Coastal Union alionyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi Nassor Mwinchui wa Pwani kwa kumpiga teke la nyuma beki wa kushoto wa Yanga Gadiel Michael.

Mara ya mwisho Yanga kupata ushindi kwenye uwanja huo ilikuwa Februari 3,2015 iliposhinda bao 1-0.



Chanzo: mwananchi.co.tz