Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Karia sasa kikaangoni

Karia Pic Data Karia sasa kikaangoni

Thu, 24 Jun 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Dar es Salaam. Kamati ya Uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limevunja ukimya baada ya rais anayetetea kiti chake, Wallace Karia kudaiwa kufanya kampeni kinyume na kanuni.

Katika kinyang’anyiro hicho Karia anapambana na Hawa Mniga na Evans Mgeusa huku wagombea Ally Salehe, Oscar Oscar na Ally Mayay Tembele wakienguliwa hatua ya awali kwa kutokidhi vigezo ikiwa ni kukosa wadhamini.

Rahim Kagenzi, Deogratias Mutungi, Abbas Tarimba na Zahoro Haji wao walichukua fomu hizo lakini hadi siku ya mwisho hawakurudisha.

Kampeni za uchaguzi huo zimepangwa kuanza Agosti Mosi hadi 6 tayari kwa uchaguzi Agosti 7, saa 6:00 usiku, ingawa hivi karibuni kumeibuka malalamiko ya baadhi ya wadau wa soka wakimlalamikia Karia kufanya kampeni kabla ya muda.

Malalamiko hayo yamekuja siku kadhaa baada ya baadhi ya watu kuvaa fulana zenye picha ya Karia katika fainali ya michuano ya vijana chini ya miaka 20 zilizofanyika hivi karibuni Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam na Mtibwa Sugar ilitwaa taji hilo kwa kuifunga Yanga, hivyo kuibua mjadala huku wengine wakitafsiri ameanza kampeni za uchaguzi kinyume na taratibu.

Akifafanua madai hayo, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Benjamin Karume alisema kuna mambo mawili kwenye tukio hilo.

Licha ya kusisitiza hawajaziona picha za tukio hilo, ingawa wanalifanyia kazi ili kubaini ukweli, alisema hata hivyo, linaweza kuwa shida kwa Karia au kinyume chake kutegemea na nafasi yake TFF hivi sasa.

“Siwezi kulizungumzia sana jambo hilo kwa sababu sijaliona na picha ya hicho kinacholalamikiwa hatujaziona, ingawa pia inaweza kuwa shida kwa Karia na vile vile inaweza pia isiwe tatizo kwani bado yupo madarakani hivyo chochote kinaweza kutokea,” alisema Karume.

Awali aliyekuwa mgombea wa urais kwenye uchaguzi huo, Ally Salehe alisema Karia amevunja kanuni kwa kuanza kampeni kabla ya muda.

Salehe wakala wa wachezaji anayetambulika na Fifa aliyeenguliwa kwenye mchakato huo kwa kutokidhi takwa la kikanuni la kuwa na wadhamini watano, alisema kitendo cha baadhi ya watu kuvaa fulana zenye picha ya Karia kwenye mashindano hayo ni kuanza kampeni kabla ya muda.

Katika mashindano hayo, mmoja wa watu aliyekuwa na jukumu la kubeba kombe alivaa fulana ya rangi ya bluu bahari yenye picha ndogo ya Karia begani huku baadhi ya wadau wengine nao wakiwa wamevaa fulana za rangi hiyo zenye picha begani ya mgombea huyo wa urais wa TFF anayetetea kiti chake.

“Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi waliangalie hilo alilofanya Karia, je? sio kampeni.

“Ingekuwa ni kipindi kingine sawa lakini hiki ni kipindi cha uchaguzi na mchakato ukiwa unaendelea na muda wa kampeni haujafika, watu wanawezaje kuvaa fulana zenye picha ya mgombea?

Kama kweli kamati inatenda haki basi wanapaswa kuchukua hatua,” alisema Salehe ambaye leo atatinga Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kufungua kesi ya kusimamisha mchakato wa uchaguzi huo ambao anadai kuna mambo mengi yamekiukwa.

Mwananchi lilimtafuta Karia ili kutoa ufafanuzi juu ya hilo, alisema hawezi kujibizana na wanatoa madai hayo kwani kipindi hiki cha uchaguzi mambo mengi yatazungumzwa.

Wakati madai hayo yakiendelea, kamati hiyo imesema hakuna mgombea yeyote aliyewekewa pingamizi na kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa TFF mtu anayeruhusiwa kuweka pingamizi ni mwanachama pekee wa mkutano mkuu.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz