Dar es Salaam.Mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu mwezi Agosti akiwashinda Joseph Mahundi na Omary Mponda.
Ofisa habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo alisema Kagere amefanikiwa kuibuka kidedea baada ya mabao yake matatu katika mechi mbili kuipatia Simba pointi sita.
"Katika kipindi hicho Kagere alifunga mabao matatu kwenye mechi dhidi ya Prisons na Mbeya City ambayo yaliifanya iwe katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
Kamati ya TFF inayosimamia utoaji wa tuzo za Ligi Kuu ilimchagua Kagere baada ya kufanya uchambuzi wa mapendekezo ya makocha waliopo katika viwanja mbalimbali.
Kagere amewashinda Joseph Mahundi ambaye katika mwezi huo aliifungia Azam FC mabao mawili na Omary Mponda wa Kagera Sugar aliyefunga mabao mawili pia.