Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kagere kila krosi bao Simba

14297 Pic+kagere TanzaniaWeb

Tue, 28 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati akiweka rekodi ya kuifungia Simba kwenye mechi tano mfululizo za mashindano, mshambuliaji Meddie Kagere amewasha indiketa katika vita ya kuwania kiatu cha ufungaji bora wa Ligi Kuu msimu huu.

Mabao mawili aliyofunga dhidi ya Mbeya City jana ni muendelezo wa kasi ya ufungaji kwa mshambuliaji huyo aliyesajiliwa na Simba akitokea Gor Mahia kwenye mechi za mashindano akiwa amefanya hivyo pia kwenye michezo minne iliyopita.

Alifunga dhidi ya JKU ya Zanzibar na Azam FC kwenye nusu fainali ya Kombe la Kagame akafunga bao kwenye mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Mtibwa Sugar, akafumania nyavu tena katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu walipocheza na Prisons kabla ya kufanya hivyo tena jana.

Katika mchezo wa jana, Kagere alitumia vyema uzembe wa mabeki wa Mbeya City kumdhibiti kufunga mabao hayo mawili kwa staili ya kupiga kichwa kwa kuchupa akiunganisha krosi mbili zilizochongwa na winga Shiza Kichuya na beki Asante Kwasi dakika ya 11 na muda wa nyongeza kwenye kipindi cha kwanza.

Mabao hayo yamemfanya Kagere afikishe idadi ya magoli matatu na kumpiku mshambuliaji wa Kagera Sugar, Omary Mponda aliyekuwa anaongoza chati ya ufungaji bora akiwa na mabao mawili.

Simba ambayo katika mchezo wa jana ilitumia zaidi mbinu ya kushambulia kutokea pembeni, ilionyesha mapema njaa ya kusaka mabao kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara langoni mwa Mbeya City ambayo kwa muda mrefu ilikuwa ikijilinda na kushambulia kwa kushtukiza.

Tofauti na mchezo dhidi ya Prisons ambayo Simba ilipata wakati mgumu, jana ilionyesha kuimarika na kucheza soka safi ikiwa na wachezaji 10 walioanza kwenye mechi ya kwanza huku Kocha Patrick Aussems akifanya badiliko moja tu kwa kumuanzisha beki Kwasi badala ya Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye alicheza mechi iliyopita.

Hata hivyo, katika dakika 25 za mwisho, Simba ilionekana kuridhika na kupunguza kasi ya mashambulizi na kuwapa mwanya Mbeya City kutulia na kufanya mashambulizi ya hapa na pale ambayo hata hivyo hayakuisaidia kusawazisha mabao hayo.

Huku ikiendelea kutomtumia kipa Deogratias Munishi ‘Dida’ ambaye hadi sasa bado hati yake ya uhamisho wa kimataifa haijafika nchini, Simba ilipata pigo dakika ya 54 baada ya kipa wake Aishi Manula kushindwa kuendelea na mchezo baada ya kupata majeraha na kulazimika kutolewa huku nafasi yake ikichukuliwa na kipa aliyepandishwa kutoka kikosi cha vijana, Ally Salim.

Ushindi huo umeifanya Simba ifikishe pointi sita na kupunguza presha ya mashabiki wake ambao wengi hawakuridhishwa na matokeo ya mchezo wa kwanza dhidi ya Prisons.

Mapema kabla ya mechi ya Simba, African Lyon iliyokuwa ugenini jijini Mwanza iliilazimisha sare ya bao 1-1 Alliance FC, matokeo ambayo yamezifanya timu zote angalau kuonja pointi ya Ligi Kuu baada ya kupoteza mechi zao za kwanza dhidi ya Stand United na Mbao FC. Simba ndio mabingwa watetezi wa Ligi Kuu.

Chanzo: mwananchi.co.tz