Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kagere atuma salamu kwa Waarabu

34899 Simbaa+pic Tanzania Web Photo

Sat, 5 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

SIMBA imeanza vizuri Mashindano ya Kombe la Mapinduzi baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Chipukizi United, katika mechi iliyofanyika Uwanja wa Amaani, usiku huu.

 

Wakitumia kikosi kilichokuwa na mchanganyiko wa wale wanaocheza mara kwa mara kikosini na wale ambao huwa hawapati nafasi, Simba walionekana kuwalazimisha Chipukizi kufunguka wakicheza soka la kasi katika kupeleka mashambulizi jambo lililowafanya wapinzani wao kuingia kwenye mkumbo wa kucheza kwa staili hiyo.

 

Mbinu hiyo ya Simba ilizaa matunda dakika ya 33, baada ya kupata bao la kuongoza kupitia kwa Meddie Kagere ambaye aliunganisha krosi nzuri ya chinichini iliyochongwa kutokea upande wa kulia na Nicholas Gyan.

 

Bao hilo lilidumu hadi wakati wa mapumziko lakini dakika tisa tu baada ya kipindi cha pili kuanza, Chipukizi waliishtua Simba baada ya kupata bao la kusawazisha dakika ya 54 kupitia kwa Omary Haji ambaye aliunganisha vyema kwa kisigino pasi iliyomkuta katika eneo la hatari la Simba.

 

Hata hivyo bao hilo lilidumu kwa dakika mbili tu kwani dakika ya 56, Simba walipata bao la pili kupitia kwa Nicholas Gyan ambaye aliunganisha kwa kichwa krosi ya Haruna Niyonzima na kuwanyanyua vitini mashabiki wa Simba waliojitokeza kwenye Uwanja wa Amaan.

Gyan aliyekuwa mwiba kwa Chipukizi kwenye mchezo huo kutokana na kasi yake ya kushambulia, alipika bao la tatu lililofungwa na Meddie Kagere mnamo dakika ya 60, baada ya kumpigia pasi safi kwenye eneo la hatari la wapinzani wao kama ambalo Mnyarwanda huyo alifunga kipindi cha kwanza.

Nahodha wa Simba, John Bocco aliyeingia kuchukua nafasi ya Kagere, aiipatia timu yake bao la nne dakika ya 82 kwa mkwaju wa penati ambao walipata baada ya Rashid Juma kuangushwa ndani ya eneo la hatari na mmoja wa mabeki wa Chipukizi.

Mbali na mabadiliko ya Bocco, Simba pia iliwaingiza Rashid Juma na Zana Coulibaly ambao walichukua nafasi za Gyan na Adam Salamba



Chanzo: mwananchi.co.tz