Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kagere alianzisha Simba

10605 Kagere+pic TanzaniaWeb

Tue, 3 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kiu ya mashabiki wa Simba kumuona mshambuliaji wao mpya, Meddie Kagere, akifanya vitu vyake, jana ilitulizwa baada ya nyota huyo kufungua rasmi akaunti ya mabao.

Kagere aliyevaa uzi wa Simba kwa mara ya kwanza, aliteremka dimbani katika mchezo wa Kombe la Kagame dhidi ya APR ya Rwanda.

Mchezaji huyo akicheza mechi yake ya kwanza, alifunga bao kwa mkwaju wa penalti dakika za nyongeza na kuipa Simba ushindi mabao 2-1.

Mkwaju huo wa penalti ulitolewa na mwamuzi Masoud Ssali wa Uganda, baada ya beki Rugwilo Herve kumuangusha mshambuliaji huyo ndani ya eneo la hatari alipokuwa akielekea kufunga.

Licha ya kufunga bao hilo, mshambuliaji huyo amethibitisha kuwa Simba haijakosea kumsajili baada ya jana kuonyesha kiwango bora akinogesha mashambulizi katika kikosi hicho.

Kagere, mzaliwa wa Uganda mwenye uraia wa Rwanda, ametua Simba baada ya kumaliza mkataba wa kuitumikia Gor Mahia ya Kenya.

Nyota huyo sasa anakwenda kutengeza pacha tatu katika safu ya ushambuliaji akiungana na akina Emmanuel Okwi na John Bocco.

Mashindano ya Kombe la Kagame huenda yakaisaidia Simba kupata majibu ya kikosi chake msimu ujao hasa kwenye safu yake ya ushambuliaji ambako kuna nyota saba wanaowania nafasi.

Suluhisho la kwanza ambalo tayari linaonekana litafanyiwa kazi msimu ujao ni kujaribu kutengeneza mazingira ya kila mshambuliaji kupata nafasi kwa kutumia mfumo wa 4-3-3 badala 3-5-2 ambao Simba ilitumia msimu uliomalizika.

Mfumo 4-3-3 unatoa nafasi kwa washambuliaji watatu kuanza kwa pamoja tofauti na 3-5-2 ambao huruhusu washambuliaji wawili kucheza pacha.

Simba ilianza kujaribisha mfumo huo katika mchezo wa kwanza dhidi ya Dakadaha kabla ya jana kuendelea nao dhidi ya APR.

Katika kile kinachotoa picha ya moja kwa moja kuwa msimu ujao Marcel Kaheza na Adam Salamba watakuwa wakishambulia kutokea pembeni, upangaji wa safu ya ushambuliaji ya Simba dhidi ya APR umetoa ishara ya moja kwa moja kuwa Mohammed Rashid atakuwa na shughuli pevu kupata namba mbele ya Bocco, Okwi na Kagere wanaocheza nafasi ya ushambuliaji wa kati.

Katika mchezo wa jana, Kaheza na Salamba waliendelea kupata nafasi ya kuanza kama ilivyokuwa kwenye mchezo wa kwanza jambo linalotoa ishara kuwa wameanza kujenga imani kwa benchi la ufundi, lakini hali itakuwa ngumu kwa Rashid ambaye alianzia benchi kumpisha Kagere.

Kaheza na Salamba walionekana kuanza kuzoeana kutokana na jinsi walivyokuwa wakipishana kila wakati kujaribu kutengeneza nafasi za mabao na kufunga, lakini hali ilikuwa tofauti kwa Kagere ambaye ameonekana bado hajamudu mfumo wa Simba.

Safu ya ulinzi na kiungo ya Simba zimeonyesha kutoathirika na ujio mpya uliofanywa kwenye usajili kwa kuwa zilikuwa na muunganiko mzuri ambao unaleta matumaini kwenye kikosi hicho msimu ujao.

Beki Pascal Wawa alishirikiana vyema na Paul Bukaba, Mohammed Hussein na Ally Shomari kuunda safu ya ulinzi iliyoweza kuhimili na kuzima kasi ya washambuliaji wa APR iliyokuwa mwiba kwa kufanya mashambulizi ya kushtukiza.

APR ilitumia mbinu ya kushambulia kwa kushtukiza ambayo nusura iwawezeshe kupata bao dakika ya 20 na 36, lakini uhodari wa safu ya ulinzi ya Simba ulioongozwa na Wawa ulikuwa kikwazo kwa Byiringilo Lague na Nshuti Dominique Savio kuipa timu yao mabao ya utangulizi.

Mambo yalionekana kugeuka kipindi cha pili na timu zote zilianza kushambuliana kwa zamu zikilenga kusaka mabao ya kuzipa pointi tatu muhimu.

Tofauti na kipindi cha kwanza, APR iliongeza kasi ya mashambulizi ikimtumia zaidi Byaringiro Lague ambaye aliwaweka kwenye wakati mgumu mabeki wa Simba.

Juhudi za APR kusaka bao zilizaa matunda dakika ya 67 baada ya Fiston Nkizingabo kumalizia kwa ustadi pasi ya Lague na kuipatia bao la kuongoza timu yake.

Awali, Lague aliwatoka Wawa na Hussein upande wa kushoto wa Simba na kupiga pasi ya chini kwa Nkizingabo ambaye alipiga kiki kali ya chini kushoto kwa kipa Ally Salim na mpira kujaa wavuni.

Simba iliongeza kasi ya mashambulizi na dakika sita baadaye Salamba aliwapatia bao la kusawazisha akimalizia shuti la Said Ndemla ambalo lilimparaza beki wa APR.

Chanzo: mwananchi.co.tz