Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kagere ajifunga Simba miaka miwili

10083 Kagere+pic TZW

Tue, 26 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mshambuliaji Meddie Kagere ameanguka saini ya kuitumikia klabu ya Simba kwa mkataba wa miaka miwili kwa gharama inayokadiliwa kufikia ya dola 60,000.

Kagere ambaye alikuwa anawindwa na Yanga, amefikia maamuzi ya kusaini mkataba huo baada ya kuwekewa ofa ya maana mezani kwake.

Mwananchi lilipojaribu kupekenyua kutaka kufahamu dau la mchezaji huyo, lilikadiliwa kufikia Dola za Kimarekani zisizopunguza 60000 kwani mchezaji huyo alikataa Dola 50000 ambazo ziliwekwa mezani na Yanga.

Tayari Simba imemnasa beki wa kati Pascal Wawa raia wa Ivory Coast, ametua Simba na anatarajiwa kuziba pengo la beki wa kigeni wa Uganda, Juurko Murshid.

Beki huyo alianza mazoezi juzi na kikosi hicho kinachonolewa na kocha Masoud Djuma kinachojiwinda na mashindano ya Kombe la Kagame, yanayotarajiwa kuanza Dar es Salaam, Juni 29.

Baada ya kumnasa Wawa, Simba imemleta Kagere aliyeng’ara katika mashindano ya SportPesa ambapo alikuwa mfungaji bora akipachika wavuni mabao manne.

Kagere mzaliwa wa Uganda mwenye uraia wa Rwanda, anayetajwa kuwa mmoja wafungaji bora Afrika Mashariki, jana alitarajiwa kutia saini mkataba wa kuitumikia Simba baada ya kumalizana na vigogo wa klabu hiyo.

Hata hivyo, usajili wa Kagere unaweza kuwa mfupa mgumu kuutafuna kwa kocha mpya wa timu hiyo kutokana na kikosi hicho kuundwa na mastaa waliotoa mchango mkubwa katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita.

Kagere atakuwa na kibarua kigumu cha kupangua kikosi bora cha nyota wawili waliounganisha pacha maridadi Emmanuel Okwi na John Bocco.

Mabao 20 ya Okwi na Bocco 14 yalitosha kuifuta machozi Simba kwa kuipa ubingwa wa Ligi Kuu, baada ya kuukosa kwa miaka sita tangu mwaka 2012.

Kutokana na rekodi nzuri ya nyota hao, Kagere atakuwa na kazi ngumu kupata namba mbele ya Bocco ambaye ni mshambuliaji halisi (namba tisa) kama ilivyokuwa kwa Kagere.

Pia, ubora wa Kagere ni tishio kwa Bocco, ambaye atalazimika kuongeza kasi ili kubaki katika kikosi cha kwanza kwa kocha mpya.

Shiza Kichuya na Okwi ndio washambuliaji pekee wenye uhakika wa namba huku wakiwa wameshikilia hatma ya wa washambuliaji wengine watatu wapya Adam Salamba, Mohammed Rashid na Marcel Kaheza.

Uwezo wa Okwi na Kichuya kucheza vyema kwenye nafasi tofauti za ushambuliaji kulingana na mifumo mbalimbali kunawapa uhakika wa namba kulinganisha na akina Bocco, Salamba, Rashid na Kaheza.

Bocco ni mshambuliaji halisi namba tisa, lakini Okwi na Kichuya wanaweza kutumika katika nafasi tofauti za ushambuliaji na wakatimiza vyema majukumu.

Kaheza na Rashid wangepata nafasi ya kucheza endapo tu wangekuwa na uwezo wa kucheza mfumo wa 4-3-3, kama washambuliaji wanaotokea pembeni.

Endapo kocha ataamua kutumia mfumo wa 3-5-2, Okwi anaonekana kuimudu vyema kwa sababu nafasi hiyo na ndio iliunda pacha hatari na Bocco.

Pia kocha akitumia mfumo wa 4-4-2 bado Kaheza, Salamba na Rashid hawatapa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza kwa kuwa Okwi anamudu vyema kucheza nyuma ya mshambuliaji na kuwaachia Bocco au Kagere mmoja kati yao kucheza namba tisa.

Kagere ametua Simba akiwa na rekodi nzuri ya kuwafunga katika mchezo wa fainali ya Kombe la Sport Pesa nchini Kenya.

Mshambuliaji huyo pia aliibuka mfungaji bora wa mashindano ya SportPes akipachika wavuni mabao matatu.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz