Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kagere aibeba Simba, Yanga hoi

52932 KAGERE+PI

Thu, 18 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tanga. Wakati nyota ya mshambuliaji Meddie Kagere wa Simba ikizidi kung’ara, Heritier Makambo jana alishindwa kuiokoa Yanga isipate kipigo kutoka kwa Mtibwa Sugar, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kagere alionyesha dhamira ya kutwaa kiatu cha dhahabu, baada ya jana kufunga mabao mawili katika mchezo ambao Simba ilishinda 2-1 dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Kagere amefikisha mabao 16 sawa na Salim Aiyee wa Mwadui Shinyanga aliyekuwa akiongoza kwa mabao muda mrefu.

Makambo alishindwa kufurukuta mbele ya ukuta wa Mtibwa na kushuhudia timu yake ikicharazwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Kabla ya mechi za jana, mshambuliaji huyo raia wa DR Congo, alikuwa akishika nafasi ya pili kwa ufungaji nyuma ya Aiyee akiwa na mabao 15.

Ushindi wa Simba katika mechi yake ya 23 ni salamu kwa Yanga katika mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.

Wakati Simba ikifikisha pointi 60, Yanga bado iko kileleni kwa pointi 74 katika mechi 32 ilizocheza katika mashindano msimu huu.

Pia Simba imeendelea vyema kula viporo vyake katika mechi zake 11 kati ya 15 zlizobaki baada ya kutolewa na TP Mazembe ya DR Congo kwa kufungwa mabao 4-1 katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga imebakiwa na mechi sita na Azam inashika nafasi ya pili kwa pointi 66, katika mechi 31 ilizocheza kwenye mashindano hayo.

Mechi zilivyokuwa

Simba ilifungwa bao dakika ya kwanza kupitia kwa Raizin Hafidhi lililotokana na makosa ya beki Erasto Nyoni na kipa Aishi Manula kuzembea kuokoa mpira.

Kagere alifunga bao la kusawazisha kwa penalti dakika ya 48 baada ya Emmanuel Okwi kuangushwa na kipa wa Coastal Union Sudi Mohammed. Pia alifunga bao la pili dakika ya 68 kwa kiki kali akimalizia pasi ya Clatous Chama.

Kwenye Uwanja wa Jamhuri, Yanga ilidondosha pointi tatu ugenini na kufikisha idadi ya mechi tatu kufungwa msimu huu. Awali, ilifungwa na Lipuli bao 1-0 kabla ya kulala 1-0 dhidi ya Stand United. Bao la Riffat Khamis alilofunga dakika ya dakika ya 52 liliendeleza rekodi bora nyumbani kwani katika michezo mitano mfululizo iliyopita iliyocheza Morogoro imeshinda yote.

Hata hivyo licha ya Yanga kuonekana mapema ingeshinda mchezo huo lakini rekodi iliwabana kwani kila mara inapokutana na Mtibwa kwenye uwanja huo inapata wakati mgumu.

Licha ya kucheza soka safi kipindi cha kwanza na kumiliki mpira kwa asilimia 51 dhidi ya 49 za Mtibwa, safu ya ushambuliaji Yanga iliyoongozwa na Makambo haikuwa makini katika kufunga.

Kipa wa Mtibwa Shabani Kado na mabeki Dickson Daudi na Cassian Ponera walifanya kazi ya ziada kuzuia mashambulizi yaliyoelekezwa langoni mwao.

Dakika ya 89 nusura liibuke zogo uwanjani baada ya Amissi Tambwe kufunga bao lililokataliwa na mwamuzi Hans Mabena baada ya mwamuzi wa pembeni kudai mfungaji aliotea.

Jambo hilo lilisababisha wachezaji wa Yanga waliokuwa uwanjani na benchi wakiongozwa na Thabani Kamusoko kumzonga mwamuzi wa pembeni wakilalamikia bao hilo.

“Waamuzi hawachezeshi kwa haki hawako upande wetu katika mechi nyingi,” alisema nahodha wa Yanga Ibrahim Ajibu.

Ajibu alisema wataendela kupambana katika michezo iliyobaki kwani licha ya wapinzani wao Simba ambao wanawafukuza wana mechi nyingi hivyo lolote linaweza kutokea. Kocha wa Simba, Patrick Aussems alisema walitumia dakika za mwanzo kuzoea uwanja aliodai haukuwa katika kiwango bora hasa eneo la kuchezea. Kocha wa Coastal Union, Juma Mgunda alisema Simba ilitumia makosa ya wachezaji wake kupata bao la kusawazisha na kufunga jingine.

Coastal: Sudi Mohamed, Miraji Adam, Adeyum Saleh, Kened Kipepa, Bakari Nondo, Said Jailan, Ayoub Lyanga, Nteje Albani, Endru Senchimbi, Raizin Hafidh na Haji Ugando.

Simba: Aishi Manula, Nicholas Gyan, Asante Kwasi, Yusuf Mlipili, Erasto Nyoni, Said Ndemla, Mzamiru Yassin, Hassan Dilunga, Meddie Kagere, Emmanuel Okwi na Haruna Niyonzima.

Mtibwa: Shaban Kado,Salum Kanoni, Issa Rashid,Dickson Daudi, Cassian Ponera,Issa Kajia, Ally Makarani, Haruna Chanongo,Salum Kihimbwa, Riphat Khamis na Jaffar Kibaya.

Yanga: Klaus Kindoki, Paul Godfrey, Gadiel Michael, Andrew Vincent, Abdallah Shaibu, Pappy Tshishimbi, Mrisho Ngasa, Thaban Kamusoko, Heritier Makambo, Erick Msagati na Raphael Daudi.



Chanzo: mwananchi.co.tz