Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kagere: Waarabu kitu gani nyie?

34065 KAGERE+PIC Tanzania Web Photo

Mon, 31 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wawakilishi wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba, wamepewa akili namna ya kuzikabili timu zote walizopangwa nazo Kundi D.

Shirikisho la Soka Afrika (CAF) liliendesha droo hiyo ikiipanga Simba kundi hilo pamoja na Al Ahly (Misri) na JR Saoura (Algeria) pamoja na AS Vita ya DR Congo.

KAULI ZA WACHEZAJI

Akizungumza na Mwananchi, mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere alisema hawawahofii Waarabu na wapo tayari kukabiliana na timu itakayokuwa mbele yao na hawana shaka na hilo.

“Lengo ni kuandika rekodi ya kimataifa. Tupo kwa ajili ya kuitumikia Simba, lakini ndio timu pekee inayoliwakilisha taifa la Tanzania, lazima tutapambana kupata matokeo na kuifikisha mbali Simba,” alisema.

Alisema kama wachezaji watapambana kufa na kupona kupata mabao na kama yeye atakachofanya ni kufunga kadiri awezavyo atakapopata nafasi.

“Waarabu sio wa kuwaogopa, tunawaheshimu kwa soka yao, lakini si wa kuogopa,” alisema Kagere mwenye mabao matatu ambayo hata hivyo alisema hafikirii sana ufungaji bora Afrika zaidi ya kutaka kuisaidia timu kufika mbali.

Kiungo wa timu hiyo Erasto Nyoni alisema saikolojia zao zinajua mwakani wana michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, jambo linalowafanya wajiamini na kuthubutu kufanya kila linalowezekana ili kuhakikisha wanaandika rekodi.

“Hatuwezi kupuuza timu ambazo tupo nazo kundi D ni gumu, tunahitaji kupambana na sio kuogopa lengo tunahitaji kupeperusha bendera ya Tanzania ili wapinzani wetu watuheshimu,” alisema.

WADAU

Mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Soka Tanzania,FAT, (sasa TFF), Muhidini Ndolanga alisema kikosi cha Simba ni kizuri isipokuwa kinahitaji kufundwa jinsi ya kulibeba taifa na sio kuonyesha maslahi binafsi ambayo hayatakuwa na mashiko.

“Ninaposema maslahi binafsi ni hivi straika anaweza akafunga bao halafu anaona mwingine ana nafasi ya kufunga anakuwa anamnyima pasi ili aendelee kushangiliwa mwenyewe na ikitokea timu ikafungwa alichokifanya kinakuwa hakina mashiko.

“Simba lazima wajue uzito wa majukumu yaliopo mbele yao, binafsi naona ina nafasi ya kufanya kitu, mfano walicheza ovyo ugenini na Nkana lakini marudiano Dar es Salaam walibadilika na wakashinda ndivyo wanavyotakiwa kufanya dhidi ya Waarabu,”alisema.

Staa wa zamani wa timu hiyo, Zamoyoni Mogella alisema wachezaji wa Simba kipindi hiki hawana njaa kama ilivyo Yanga, hivyo wanatakiwa kuonyesha umafia kimataifa na kuweka dhamira ya kuwaonyesha Waarabu kama inatosha kuwaonea.

“Kila timu inaingiza wachezaji 11 uwanjani, Simba hatupaswi kutazama rekodi jinsi walitufunga kipindi cha nyuma, tuna kikosi kizuri cha wachezaji wanaojitambua kikubwa ni kukaa nao kuwaeleza wanaliwakilisha taifa.

“Ugumu wa timu hizo unakuja vile unavyouchukulia lakini ukisema naweza kufanya kitu hiki kinafanikiwa kwani wao wana maajabu gani, Simba ijiamini isipokuwa mabeki na washambuliaji waongeze umakini,” alisema. Nahodha wa zamani wa timu hiyo, Mussa Mgosi aliwataka washambuliaji wa timu hiyo kuacha akili za kutaka washangiliwe na mashabiki, kitu alichokiona ndicho chanzo cha ubinafsi.

“Inashangaza pale unapowaona wachezaji wanaanza kushangilia kabla hajafunga hata bao, hilo linaonyesha ni kiasi gani wanataka kuwa mastaa pasipo kutimiza malengo ya klabu, Simba ina nafasi watulize akili zao,” alisema.



Chanzo: mwananchi.co.tz