Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kagere, Chama awabebeshwa zigo

51711 Kagere+pic

Thu, 11 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

WAKATI mabosi wa Simba chini ya Mtendaji Mkuu wao, Crescentius Magori wapo bize kupambana na Shirikisho la Soka Afrika (Caf) juu ya ishu ya waamuzi wa mechi yao ya marudiano na TP Mazembe, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Patrick Aussems amecheka akidai kuna kila dalili ya Wakongomani kuanza kuihofia Simba, naye akafanya mambo kwa kuwabebesha zigo kina Meddie Kagere na Clatous Chama.

Aussems amesema mbinu atakazotumia kwenye mchezo huo wa marudiano utakaochezwa Jumamosi zitawashangaza Wakongo nyumbani kwao, licha ya kukiri ni pambano gumu kwelikweli.

Kocha huyo alisema wamegundua kwenye mchezo wa kwanza viungo wao walishindwa kumiliki mpira na washambuliaji kupoteza nafasi nyingi kizembe na kuwapa nafasi Mazembe kuwatawala, lakini wanapoenda kuwafuata kwao viungo wake na washambuliaji watakuwa na kazi maalum Lubumbashi.

Sikia sasa. Jana Jumatano saa 5:30 asubuhi katika mazoezi ya kwanza ya ufundi ya kikosi cha Simba, kocha Aussems na msaidizi wake Denis Kitambi waligawana, Kitambi akiwachukua mabeki wa pembeni akiwaonyesha jinsi krosi za siku hiyo zinavyotakiwa kupigwa.

Hapo hakukuwa na utani ukikosea unapigwa somo la maana ambalo mabeki Asante Kwasi, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na Zana Coulibaly walikuwa wakihenyeshwa kuhakikisha krosi zao zinakuwa bora kuelekea mechi hiyo.

Upande wa pili, Aussems aliwachukua viungo, mabeki wa kati na washambuliaji kisha akawa anawapa makali ya kile wanachotakiwa kukifanya wanapopata mpira na wanapopoteza.

Mbelgiji huyo amesisitiza anataka kuona washambulaiji wake wanakuwa na kasi katika kuharakisha kufika lango la wapinzani na wakifika hapo hakuna zaidi ni kumchambua kipa lakini pia viungo wa kati wametakiwa kutopoteza pasi hovyohovyo.

Katika umakini huo, Aussems jana nusura awe mbogo kwa kiungo wake Said Ndemla akitaka kumuona anakuwa na pasi za haraka huku akicheza kwa umakini mkubwa akifanya mawasiliano na wenzake kazi ambayo pia alitaka kuiona inafanywa na viungo wengine.

Mabeki wa kati nao pamoja na kipa wametakiwa kuwa makini lakini pia kuwa na jicho la mbali la kuwapanga wenzao mara wanapopoteza mpira ili mashambulizi ya wapinzani wao yasifike kwa haraka langoni mwao.

MSIKIE MWENYEWE

Akizungumzia mchezo huo utakaopigwa pale Uwanja wa Mazembe jijini Lubumbashi, Aussems alisema mbinu za kuanza kubadilisha mwamuzi hazijamshtua lakini anaona ni jinsi gani Mazembe inawaogopa Simba.

“Huu ndio mpira wa Afrika sijashtuka sana lakini ninachoona mimi ni kwamba wapinzani wetu wanajua Simba ni timu ya aina gani na wanaiogopa ni marafiki kule najua wanachozungumza kuhusu sisi na inatupa nafasi ya kuwafuata na mbinu mpya ili kuwamalizia kwao,” alisema Aussems.

Aussems alisema tangu kuanza kwa hatua ya makundi hawajashinda ugenini, lakini mchezo ujao Simba itakuwa tofauti na ile ambayo wengi wameiona katika mechi zilizopita kwani anawaandaa vijana wake kuwalazimisha Mazembe wafanye makosa langoni mwao ili wawamalize.

“Hatutakiwi kufanya makosa ya kupoteza mpira katika sehemu ya kiungo, pia tukienda mbele tutatakiwa kuwa na malengo makubwa tutawalazimisha wafanye makosa, tuko katika utofauti mkubwa ukilinganisha na mechi za nyuma tulizocheza ugenini.”

Aidha Aussems alisema katika safari yao ya kesho alfajiri kuwafuata Mazembe anataka kuondoka na jeshi la wachezaji 18 pekee lakini nani atabaki na nani ataenda atajua kesho kwani anataka kujiridhisha. Uamuzi huo wa Aussems unatokana na jana kiungo wake mkabaji James Kotei kupata maumivu kidogo ingawa alionekana kupata matibabu mazuri kuelekea mechi hiyo.

Pia awali Aussems alitaka kufanyia mazoezi katika Uwanja wa nyasi za bandia za kituo cha Jakaya Kikwete kilichopo Kidongo Chekundu lakini wakakosa na kocha huyo alionyesha kusikitishwa na hilo.

“Unajua kule tunakwenda kutumia uwanja wa nyasi bandia sasa nilitaka tukafanyie mazoezi pale nasikia tumekataliwa, ila hakuna shida changamoto kama hizi ndio zitatupa morali. ”

BOCCO MZUKA

Nahodha wa Simba John Bocco alisema wachezaji wanzake wana morali kubwa ya kushindana katika mechi ya marudiano.

Bocco alisema kuhusu kubadilishwa kwa waamuzi ambao walipangwa kuchezesha mchezo huo, wachezaji hawataki kuliweka akilini, wanafikiria kazi yao ya kwenda kupambana ndani ya dakika 90.

“Makocha wetu wanaendelea kutuelekeza na kutupa mbinu ambazo naamini ndizo tutatumia katika mechi ya marudiano bila shaka Mungu akitutangulia wachezaji wote tukiwa wazima na salama.”



Chanzo: mwananchi.co.tz