IKIWA katika dakika za lala salama, Ligi Kuu Bara leo itaendelea kwa mchezo mmoja utakaopigwa saa 10:00 za jioni kwenye dimba la Kaitaba ambapo wenyeji Kagera Sugar watakuwa wakiikaribisha Ruvu Shooting.
Ni mechi inayotarajiwa kuwa ya kibabe zaidi kulingana na kila timu kutaka alama tatu zitakazoisogeza juu kwani hadi sasa timu hizo zimebakiza takribani mechi tano na bado hakijaeleweka.
Kagera ipo nafasi ya pili kutoka mkiani (17), ikiwa na alama 30 baada ya kucheza mechi 29 huku mpinzani wake Ruvu akiwa nafasi nane na alama 37 alizovuna kwenye michezo 28.
Tofauti ya pointi kati ya timu hizo mbili ni alama saba pekee jambo ambalo Kagera ikishinda leo itakuwa imebakiza pengo la alama nne na itafikisha alama 33 zitakazoipandisha hadi nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi.
Ruvu nao wataingia uwanjani wakizitaka alama tatu kwa udi na uvumba ili kuendelea kujihakikishia kubaki Ligi Kuu kwa msimu ujao huku wakiifukuzia nafasi ya tano kimya kimya kwani atafikisha alama 40, moja nyuma ya KMC iliyo nafasi ya tano na alama 41.
Kwa mara ya mwisho timu hizi mbili kukutana kwenye ligi ilikuwa Novemba 29, mwaka jana ambapo Ruvu walikuwa wenyeji na mechi kumalizika kwa suluhu (0-0).